Harakati za kuwasambaratisha Taliban
4 Februari 2010Hatua hiyo ina azma ya kuepusha nchi hiyo kutengwa na Afghanistan, ambayo India inaona ni muhimu kwa usalama wake.
Maafisa nchini India wana wasiwasi kwamba, mpango huo wa Afghan ulioidhinishwa na mataifa yenye nguvu duniani, kuwashinda wapiganaji wa Taliban, utaweza kumpa sauti kubwa mpinzani wao Pakistan katika juhudi za kuleta amani na kwamba hatimaye unaweza kuliongoza kundi la Taliban kuchukua uongozi, mara majeshi ya nchi za magharibi yatakapoondoka nchini Afghanistan.
Upinzani uliopo kati ya India na Pakistan ambao umedumu kwa miongo sita, tangu uhuru wao kutoka kwa Mwingereza mwaka 1947, umeigeuza Afghanistan kuwa uwanja wa mapambano wa wawakilishi wake, ambapo nchi zote zinaona muhimu kwa maslahi yao.Wapinzani hao wawili India na Pakistan wanaelezwa kuwa wamekuwa wakitatiza juhudi za magharibi kuimarisha Afghanistan.
Maelewano na Taliban
Wito wa Rais wa Afghanistan Hamid Karzai kuitaka Saud Arabia na Pakistan kusaidia kuleta maelewano na Taliban, kunatishia kufuta rasilimali za miaka minane za fedha na kidiplomasia zilizoipa India sauti kubwa kwa Afghanistan.Mtaalamu wa sera za nje Raja Mohan anasema kushindwa kwa India kupokea hali ya mabadiliko nchini Afghanistan kunaweza kusababisha kizuizi kikubwa kwa nchi hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa India alisema kuwa nchi yake ina nia ya kuunga mkono juhudi za kutafuta amani na Taliban ili kuiimarisha nchi hiyo jirani yake, Afghanistan.
Kwa upande wake utawala wa Rais Karzai wa Afghanistan una shaka kuhusu Pakistan, ambayo inaizingatia Afghanistan kama maficho yao iwapo kutatokea vita vingine na India na kwa sababu Pakistan inaushirikiano na Taliban.
Masomo kwa ajili ya amani
India imekuwa ikitafuta kuweka ushawishi wake kwa Afghanistan ili kuzuia kambi zozote za mafunzo za wapiganaji wanaoipinga nchi hiyo, ambapo imekuwa ikidai kuwa mpinzani wake Pakistan ndio amekuwa akiwaunga mkono wapiganaji hao.Katika kuimarisha uhusiano wake huo na Afghanistan, India hivi karibuni ilitangaza pia kutoa ufadhili kwa wanafunzi kadhaa wa Afghanistan wanaosomea masomo ya kilimo, sekta ambayo kwa sasa inaonekana muhimu katika kuimarisha maisha ya Waafghan.
Maafisa nchini India wamesema nchi hiyo siku zote imekuwa mshirika wa maendeleo wa Afghanistan na kwamba ufadhili huo uliotoa utaimarisha zaidi uhusiano wao.
Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters)
Mhariri:Abdul-Rahman