1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za kujenga uongozi wa wanawake Somalia

Mohmed Dahman8 Septemba 2008

Kundi la wanawake 60 wa Kisomali limekuwa na kikao cha wazi cha aina yake wiki iliopita kushirikiana mawazo juu ya dhima ya mwanamke katika mchakato wa amani katika nchi yao ilioathirika na vita .

https://p.dw.com/p/FDGm
Machafuko bado yanaendelea katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu.Picha: picture-alliance/ dpa

Somalia imekuwa haina serikali inayofanya kazi ipasavyo tokea mwaka 1991.

Wanawake wa Somalia walikutana katika mji wa Bagamoyo ulioko kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi nchini Tanzania wiki iliopita.

Miaka kumi na saba ya mzozo wa kiraia,uhaba mkubwa wa chakula kutokana na ukame wa mara kwa mara na umaskini unaozidi kukithiri kumesababisha kile Umoja nwa Mataifa inachokiita kuwa maafa makubwa kabisa ya kibinaadamu duniani.

Kwa kupitia hali hiyo yote wanawake katika nchi hiyo ya kihafidhina ya Pembe ya Afrika kwa kiasi kikubwa wamezuiliwa kuelezea upinzani wao.

Katika mahojiano na shirika la habari la IPS Zahra Mohamed wa shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake mjini Nairobi Kenya la Jinsia,Elimu,Uongozi na Kuwaezesha Wanawake amesema vita vinaendeshwa na wanaume na ni wanaume wenye kuongoza siasa nchini mwao.

Amesema wanawake wanaojihusiha na siasa ni wachache sana na sauti zao sio kubwa sana wengi wao wanahaha kujipatia usalama wa kila siku,chakula na kazi za kila siku kwamba hawana muda wa kufanya jambo jengine.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Taasisi ya Utafiti na Mafunzo kwa ajili ya Kuwaendeleza Wanawake ya Umoja wa Mataifa UN- INSTRAW kwa ufupi wanawake takriban wametolewa kabisa katika mchakato wa amani na kujenga taifa nchini Somalia.

Inaripotiwa jambo hilo limeanza kubadilika taratibu.

Mwaka huu kumekuwepo na jitihada mpya za kuwahusisha wanawake wa Somalia katika kuleta utulivu kwa nchi yao kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2009 ambao yumkini ukaahirishwa kutokana na hali ya usalama kutokuwa thabiti.

Semina mbili zilizowakusanya wanawake waliomo kwenye serikali ya mpito ya Somalia pamoja na kutoka ndani ya nchi hiyo na wale wanaoishi nchi za nje zilifanyika nchini Italia mapema mwaka huu.Kama vile mkutano wa wiki iliopita wa Bagamoyo ziliandaliwa na UN -INSTRAW na Chama cha Wasomali walioko Nje na Amani ADEP chenye makao yake mjini Milan Italia ambapo serikali ya Italia ilidhamini.ADEP kinashughulikia haki za wahamiaji wa Somalia nchini Italia na kuwawezesha wanawake nchini Somalia.

Carolina Toborga kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti na Mafunzo ya Umoja wa Mataifa ya Kuwaendeleza Wanawake UN-INSTRAW yenye makao yake huko Santo Domingo Jamhuri ya Dominika amesema wanjarivbu kuwasaidia wanawake wanaoshi nchini Somalia kuanza kujenga ushirikiano na wanawake wenzao wa Somalia wanaoishi nchi za nje ambao wana rasimali kusaidia kuleta mabadiliko ndani ya nchi na kuwa na mahusiano na jumuiya ya kimataifa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwa wastani wanawake 45 hufariki kila siku nchini Somalia wakati wa kujifunguwa na kiwango cha wasichana wanaoandikishwa shule cha asilimia 15 ni mojawapo ya kiwango cha chini kabisa barani Afrika.

Mapambano kati ya vikosi vya serikali ya Somalia na makundi ya upinzani yenye silaha yamesababisha takriban watu milioni moja kukimbia makaazi yao ndani ya nchi ,zaidi ya Wasomali milioni tatu wameomba hifadhi katika mataifa ya Kiafrika,Ghuba ya Uajemi,Australia na Amerika Kaskazini.

Katika hali ya kutokuwepo kwa utawala wa sheria kwa jumla ubakaji na aina nyengine za dhuluma vimekuwa vikiongezeka kama mbinu inayotumika kwa makusudi kwenye mizozo.

Mojawapo ya dhamira kuu ya mazungumzo hayo yanayodhaminiwa kimataifa kwa ajili ya wanawake wa Somalia ni kusaidia kutekeleza Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1325 ambalo linaelezea hatua za kuboresha dhima ya wanawake katika kujenga amani.