1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harakati za Afrika kudhibiti migogoro

30 Desemba 2012

Uasi wa kabila la Tuareg nchini Mali uliokuja kusababisha mapinduzi na uasi wa Waislamu wa itikadi kali vimehanikiza bara la Afrika mwaka 2012 pamoja na kuzuka upya kwa umwagaji damu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

https://p.dw.com/p/17BNP
Umoja wa Afrika
Umoja wa AfrikaPicha: dapd

Barani kote Afrika mwaka 2012 kulizuka upya mizozo juu ya ardhi, rasilmali,dini na madaraka ilioanza kutokota au kumalizikia kwa amani ilio tete.Rais wa Mali alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi hapo mwezi wa Machi kutokana na wananchi kutoridhika kwa namna alivyokuwa akiushughulikia uasi wa Tuareg.Katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja baada ya hapo Watuareg walilitangaza eneo la kaskazini kuwa taifa huru. Lakini Waislamu wa itikadi kali waliinyakua miji muhimu katika eneo hilo na kuanzisha sheria za Kiislamu 'Sharia'.Mapigano katika pande tatu yamepelekea maelfu ya watu kukimbia na kuzusha wasi wasi kwa jumuiya ya kimataifa.Umoja wa Mataifa umeidhinisha kutumwa kwa kikosi kitakachoongozwa na Afrika kuisaidia serikali ya Mali kulikombowa eneo la kaskazini.

Waasi wa kundi la M23 wakiwa mashariki ya Congo.
Waasi wa kundi la M23 wakiwa mashariki ya Congo.Picha: AP

Maelfu wakimbia mapigano

Nako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mapigano kati ya kundi jipya la waasi na jeshi la Congo yamesababisha kukimbia mamia kwa maelfu ya watu tokea mwezi wa Aprili.Hapo mwezi wa Novemba kundi la M23 liliushikilia kwa muda mfupi mji wa Goma na uwanja wa ndege wake. Hata hivyo pande hizo mbili kufuatia ombi la viongozi wa kanda ya Maziwa Makuu zimekubali kuwa na mazungumuzo.Kwa kiasi kikubwa kundi la M23 linaundwa na watu wa kabila la Watutsi walioasi jeshini wenye mahusiano na nchi jirani ya Rwanda.

Umoja wa Mataifa umezitaka Rwanda na Uganda kutoliunga mkono kundi hilo la M23 na kuheshimu vikwazo vya silaha dhidi ya Congo.Umeitaka serikali ya Rwanda inayodhibitiwa na Watutsi kutumia ushawishi wake kwa waasi hao kutafuta amani.Nchi zote mbili zimekanusha madai ya kuliunga mkono kundi hilo.Kuenea kwa mzozo wa mauaji ya kimbari ya Rwanda katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati yenye utajiri wa madini lakini isiokuwa na utulivu wa kisiasa kumechochea vita vya maafa makubwa kuwahi kushuhudiwa barani Afrika ambapo inakadiriwa watu milioni tano walipoteza maisha yao.Hata hivyo uhasama umezuka tena tokea kutiwa saini kwa makubaliano ya amani ya mwaka 2003.

Mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa katika doria mashariki ya Congo.
Mwanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa katika doria mashariki ya Congo.Picha: dapd

Kikosi cha kimataifa kutumwa Congo

Umoja wa Afrika hivi sasa unajadili mpango wa kutuma kikosi kipya cha kimataifa cha kulinda amani katika eneo tete la mashariki mwa Congo wakati nchi jirani zikiwa na wasi wasi kwamba mzozo huo wa Congo utasambaa na kuingia nchini mwao.Umoja wa Mataifa ukiwa na kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani 20,000 huko Congo kimeshutumiwa kwa kushindwa kukomesha unyama unaofanywa na waasi.

Baadhi ya wachambuzi wanaishutumu mipango ya Umoja wa Afrika kutuma vikosi huko Congo na Mali.Alfred Tijurimo Hengari mtafiti wa Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Afrika Kusini anasema mataifa husika katika kanda mara nyengine yanakuwa sehemu ya tatizo ambapo katika kesi ya Congo kuna nchi kwenye kanda hiyo ambazo zimezama kwenye mzozo huo.

Naye mtafiti katika Chuo cha Masomo ya Mashariki na Kiafrika kilioko London Jeremy Keenan anasema uingiliaji kati wa kijeshi wa aina yoyote ile nchini Mali utaifanya hali kuzidi kuwa mbaya.Kikosi cha kuingilia kati kijeshi nchini Mali kinatarajiwa kuwa na wanajeshi 3,300 kutoka nchi za Jumuiya ya Ushikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS. Keenan hadhani kwamba Umoja wa Afrika unafaa kuuongoza operesheni hiyo ambayo angalau inahitaji mwaka mmoja kuwapatia mafunzo wanajeshi wake, masuala anayojiuliza ni pamoja na nani watakaowapatia mafunzo na kulipia gharama zake. Anasema atashangaa iwapo operesheni hiyo itaweza kufanyika kweli.

Waasi wa kabila la Tuareg walipoliteka eneo la kaskazini mwa Mali.
Waasi wa kabila la Tuareg walipoliteka eneo la kaskazini mwa Mali.Picha: picture alliance/Ferhat Bouda

Hali ya Somalia inatia moyo

Somalia ambayo iliwahi kuelezewa kuwa ni taifa lililoshindwa kujiendesha imepata mafanikio makubwa dhidi ya waasi wa itikadi kali za Kiislamu wenye mafungamano na kundi la Al -Qaeda kutokana na msaada wa kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM kilichowekwa nchini humo tokea mwaka 2007.Hapo mwezi wa Septemba baada ya sehemu kubwa ya mji mkuu wa Mogadishu kutangazwa kwamba imekombolewa wabunge wa Somalia wamemchagua rais mpya kuingoza serikali inayofanya kazi kikamilifu ambayo imekuwa ikokosekana nchini humo kwa miongo kadhaa.

Kikosi cha AMISOM kinacholinda amani Somalia.
Kikosi cha AMISOM kinacholinda amani Somalia.Picha: AP

Baadhi ya watu wanayaona mafanikio ya AMISOM kuwa hafifu,Hengari anatahadharisha dhidi ya kupitisha mpango kama huo kuweka kikosi kama hicho mahala pengine Afrika. Anasema majeshi ya Afrika hayakupatiwa mafunzo mazuri,hayana silaha na kwa hiyo kuna haja ya kuchambuwa upya mfumo wake wa kulinda amani.Likija katika suala la uwanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu hata Kenya ambayo kwa wastani ni nchi imara imeshuhudia mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa kuisaidia Somali kuwaondowa Al-Shabaab.

Nchini Nigeria takriban watu 200 wameuwawa katika mashambulizi kadhaa ya mabomu yaliofanywa na kundi la Boko Haram kaskazini mwa nchi hiyo ambapo kundi hilo linataka kuanzisha sheria za Kiislamu "Sharia".Sudan na Sudan Kusini nusura zitumbukie vitani kutokana na mzozo wa ada za mafuta na mipaka hapo mwezi wa April.Umoja wa Mataifa uliamuru kukomeshwa kwa mapigano na kuondolewa kwa vikosi kwenye eneo la mpakani la mkoa wa Abyei. Wasudani bado kutekeleza makubaliano ya amani yaliofikiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika hapo mwezi wa Septemba.

Mabaki ya pikipiki ya mojawapo ya mashambulio ya kujitowa muhanga ya Boko Haram huko Bauchi Nigeria.
Mabaki ya pikipiki ya mojawapo ya mashambulio ya kujitowa muhanga ya Boko Haram huko Bauchi Nigeria.Picha: picture-alliance/dpa

Mwandishi:Mohamed Dahman/dpa

Mhariri:Ssessanga,Iddi Ismail