Hamilton ashinda mbio za Grand Prix za Uingereza
17 Julai 2017Dereva wa Ferrari Sebastian Vettel alikuwa na bahati mbaya baada ya gurudumu lake kupata pancha katika mzunguko wa mwisho na hivyo kuupunguza uongozi wa wa ubingwa wa dunia kwa pointi moja. Hamilton aliongoza toka mwanzo hadi mwisho katika siku ambayo mwenzake wa timu ya Mercedes Valtteri Bottas alimaliza katika nafasi ya pili. Vettel ambaye alimaliza katika nafasi ya saba wakati mwenzake wa Ferrari Kimi Raikonnen akimaliza katika nafasi ya tatu.
Hamilton ndiye dereva wa tatu, baada ya Muingereza mwenzake marehemu Jim Clark na Mfaransa Alain Prost, kushinda mbio za Grand Prix za Uingereza mara tano na wa kwanza kupata ushindi mara nne mfululizo katika mashindano hayo ya Uingereza. "Ni hisia nisizoweza kuelezea. inafurahisha sana kuwa hapa jukwaani. nnajivunia sana kuona bendera hizi kila mahali na mashabiki wamejitokeza kwa wingi. nnajivunia saan kuwa nimeshinda kwa ajili yenu. ahsanteni sana kwa msaada wenu kwa kutusukuma. timu yangu imefanya kazi nzuri. Valtteri alifanya kazi nzuri pia, hivyo ni wikendi nzuri sana kwetu".
Bila shaka mashabiki wa Formula One wanasubiri kwa hamu kuona kivumbi kitakachotokea kati ya Hamilton na Vettel katika mkondo wa Grand Prix nchini Hungary baadaye mwezi huu.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu