HAMBURG: Majengo ya washukiwa kuhusika na ugaidi yasakwa
10 Mei 2007Kama wafuasi 6,000 wa mrengo wa shoto wamendamana katika miji mbali mbali nchini Ujerumani kupinga msako mkuu unaofanywa na polisi katika maandalizi ya mkutano wa kilele wa nchi tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8.Katika mji wa Hamburg,waandamanaji walipambana na polisi na idadi kadhaa ya watu walijeruhiwa.Kwa upande mwingine,maandamano yaliyofanywa Berlin,Cologne,Hannover na miji mingine yalikwenda kwa amani.Siku ya Jumatano, polisi katika mji mkuu Berlin na kaskazini mwa Ujerumani,waliamriwa kusaka jumla ya nyumba na ofisi 40 zinazotumiwa na wafuasi wa mrengo wa shoto,lakini hakuna aliekamatwa.Kwa mujibu wa ofisi ya mwanasheria wa serikali,wafuasi 21 wa mrengo wa shoto wanashukiwa kuwa wameunda kundi la kigaidi kwa azma ya kufanya ghasia au watajaribu kuzuia mkutano wa kilele wa G-8 uliopangwa kufanywa mjini Heiligendamm mnamo mwezi wa Juni.