1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hamas yasema itaendelea na mazungumzo ya usitishaji vita

7 Machi 2024

Wanamgambo wa Hamas wamesema wataendelea na mazungumzo kupitia wapatanishi hadi pale watakapofikia makubaliano ya kusitisha vita na Israel.

https://p.dw.com/p/4dFiD
Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas Osama Hamdan (Picha ya maktaba)
Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas Osama Hamdan (Picha ya maktaba)Picha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

Kwenye taarifa, wanamgambo wa Hamas wamesema wataendelea na mazungumzo kwa lengo la kusaka makubaliano yatakayoafiki matakwa na masilahi ya watu wao.

Imeongeza kuwa imeonesha utayari unaohitajika kufikia maelewano yanayohitajika ili kukomeshwa kwa kile walichokitaja "uchokozi" huko Gaza.

Kundi hilo la wanamgambo ambalo Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha miongoni mwa makundi ya kigaidi, limeishutumu Israel likisema imeweka vizingiti katika mazungumzo hayo.

Kwenye taarifa yake, Hamas imesema Israel ingali inakwepa hoja kuu za makubaliano hususani zile zitakazowezesha usitishaji kabisa wa vita, kujiondoa katika Ukanda wa Gaza, kuwezesha waliokimbia mapigano kurejea makwao na kuwapa wakaazi wa Gaza mahitaji yao.

Soma Pia: Juhudi za kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza zaendelea

Wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar, wako Cairo pamoja na wawakilishi wa Hamas, wakiendelea na mazungumzo ya makubliano ya usitishaji vita kwa muda.

Israel haishiriki moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin NetanyahuPicha: Ronen Zvulun/AFP/Getty Images

Israel yataka kujua mateka ambao wangali hai

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anawataka wanamgambo wa Hamas kuchapisha orodha ya majina ya mateka wanaowashikilia huko Gaza ambao bado wangali hai.

Lakini maafisa wa Hamas wamesema hawawezi kusema mateka waliokamatwa Israel ambao wangali hai kutokana na mashambulizi ya Israel.

Hamas na makundi mengine ya wanamgambo ya Palestina, waliwashika mateka takriban watu 240, waliposhambulia kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7 katika mkasa ambao watu wapatao 1,200 waliuawa.

Israel ilijibu shambulizi hilo kwa kutangaza vita dhidi ya Hamas, ambapo imekuwa ikiushambulia vikali na mara kwa mara Ukanda wa Gaza, kufunga eneo la pwani ya Palestina huku wanajeshi wake wakifanya operesheni ndani ya Gaza kwa lengo la kuwaondoa Hamas.

Maafa Gaza yazidi kuongezeka

Kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka kwa wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, watu 30,717 wameshauawa ndani ya Gaza na 72,156 wengine wamejeruhiwa tangu vita hivyo vilipoanza.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Soma pia: Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza

Hali ya kibinaadamu ndani ya Gaza imegeuka kuwa janga baada ya karibu miezi mitano ya mapigano. Miito ya jumuiya ya kimataifa imekuwa ikiongezeka kwa Israel kuruhusu misaada zaidi kuingia kwenye Ukanda huo.

Kulingana na ripoti za vyombo vya habari, kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza, serikali ya Israel inatarajiwa kuruhusu meli kupeleka misaada Gaza.

Mipango ya kusafirisha misaada kwa meli pia ilithibitishwa mnamo Jumatano na msemaji wa rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, huko Brussels.

China: Vita vya Gaza ni "aibu kwa ustaarabu"

China imevitaja vita vya Gaza kuwa "aibu kwa ustaarabu" na imetaka mapigano kusitishwa mara moja. Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alipozungumza na waandishi babari mjini Beijing. Alisikitika kwamba kadhia hiyo imeshindwa kukomeshwa katika karne ya 21.

Rais wa Marekani Joe Biden amewataka Hamas kukubali mpango wa kusitisha mapigano na Israel kabla ya mwezi wa mfungo wa Ramadhani, ambao unaweza kuanza Jumapili.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa baa la njaa linawanyemelea Wapalestina ambao wamezongwa na mapigano.

Bonyeza linki ifuatayo kwa makala mbalimbali kuhusu Mzozo wa Israel na Hamas.

Vyanzo: DPAE, AFPE