Hamas yaikosoa Marekani kuidhinisha msaada kwa Israel
21 Aprili 2024Msaada huo kwa kiasi kikubwa utaiimarishamifumo ya ulinzi wa angani ya Israel.
Hamas ambalo linachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi kadhaa za Magharibi, imesema katika taarifa kuwa msaada huo ambao unakiuka sheria za kimataifa, ni idhini ya serikali ya itikadi kali ya Israel kuendeleza vita vyake.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Natanyahu amesema muswada huo wa msaada ulioidhinishwa unaonyesha uungwaji mkono kwa Israel. Hapo jana, Baraza la Wawakilishi la Marekani liliidhinisha kitita cha dola bilioni 13 katika msaada wa kijeshi kwa Israel ambayo ni mshirika wa kihistoria wa Marekani, katika vita vyake dhidi ya Hamas huko Gaza.
Hayo yanajiri wakati Israel ikiendeleza mashambulizi yake kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah. Hospitali ya Kuwait mjini Rafah imesema watu 18, wakiwemo watoto 14 waliuawa katika mashambulizi ya jana usiku.