1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamas, Islamic Jihad wakataa pendekezo la kuachia madaraka

25 Desemba 2023

Hamas na Islamic Jihand wamekataa pendekezo la Misri kwamba waachie madaraka Gaza ili kuwapo na usitishaji wa kudumu wa mapigano, duru za Misri zimesema.

https://p.dw.com/p/4aZfW
Ukanda wa Gaza | Kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar
KIongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza, Yahya Sinwar.Picha: Ashraf Amra/ZUMAPRESS/picture alliance

Makundi yote mawili, ambayo yamekuwa yakifanya mazungumzo tofauti na wapatanishi wa Misri mjini Cairo, yalikataa kutoa muafaka wowote zaidi ya uwezekano wa kuachiliwa kwa mateka zaidi waliokamatwa Oktoba 7 wakati wapiganaji walipoingia kusini mwa Israel, na kuua watu 1,200.

Misri ilipendekeza "mapango", ambao pia unaungwa mkono na wapatanishi wa Qatar, ambao ungehusisha usitishwaji wa mapigano ili kubadilishana na kuachiliwa kwa mateka zaidi, na kusababisha makubaliano mapana zaidi ya usitishaji wa kudumu wa mapigano pamoja na mabadiliko ya uongozi katika Ukanda wa Gaza, unaoogozwa kwa sasa na Hamas.

Yoav Gallant | Waziri wa Ulinzi wa Israe na Yahya Sinwar| Mkuu wa Hamas
Waziri wa ulinzi wa Israel Yoav Gallant, kushoto, na Kiongozi wa Hamas katika Ukanda wa Gaza Yahya Sinawar.Picha: AFP

Misri ilipendekeza uchaguzi huku ikitoa uhakikisho kwa Hamas kwamba wanachama wake hawatafukuzwa au kufunguliwa mashitaka, lakini kundi hilo lilikataa makubaliano yoyote isipokuwa kuachiliwa kwa mateka, vyanzo vilisema. Zaidi ya mateka 100 bado wanaaminika kushikiliwa Gaza.

Soma pia;Mashambulizi ya Israel yaua 100 katika mmoja ya usiku mbaya zaidi wa vita Gaza 

Afisa wa Hamas ambaye alitembelea Cairo hivi karibuni alikataa kuzungumzia moja kwa moja mapendekezo makhsusi ya usitishaji mapigano wa muda wa kibinadamu na alionyesha kukataa kwa kundi hilo kwa kurudia msimamo wake rasmi.

"Hamas inataka kukomesha uonevu wa Israel dhidi ya watu wetu, mauaji na mauaji ya halaiki, na tulijadiliana na ndugu zetu wa Misri njia za kufanya hivyo," afisa huyo aliiambia Reuters.

"Tulisema pia kwamba msaada kwa watu wetu lazima uendelee na lazima uongezeke na lazima uwafikie wakazi wote wa kaskazini na kusini," afisa huyo alisema.

"Baada ya uvamizi kusitishwa na misaada kuongezeka tuko tayari kujadili ubadilishaji wa wafungwa," aliongeza.

Msimamo wa kundi la Islamic Jihad

Kundi la Islamic Jihad, ambalo pia linashikilia mateka Gaua, limetoa msimamo sawa na huo.

Soma pia: Kiongozi wa Hamas awasili Misri kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza

Ujumbe wa Islamic Jihad ulioongozwa na kiongozi wake Ziad al-Nakhala hivi sasa uko mjini Cairo kubadilishana mawazo na maafisa wa Misri kuhusu kubadilishana wafungwa na masuala mengine, lakini afisa mmoja alisema kundi hilo lilikuwa limetaja ukomeshaji wa mashambulizi ya kijeshi ya Israel kama sharti la majadiliano zaidi.

Vikosi vya Israel vyaonesha silaha zilizofichwa katika mdoli

Islamic Jihad inasisitiza, alisema afisa huyo, kwamba ubadilishanaji wowote wa wafungwa laazima ufanyika kwa msingi "wote kwa wote", ikimaanisha kuachiwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa Gaza na Hamas na Islamic Jihad, kwa kubadilishana na Wapalestina wote walioko katika jela za Israel.

Kabla ya vita, kulikuwa na Wapalestina 5,250 katika jela za Israel, lakini idadi hiyo imeogezeka hadi takribani 10,000 baada ya Israel kukamata maelfu zaidi katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, kulingana na chama cha wafungwa wa Kipalestina.

Chanzo: RTRE