1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali yatatanisha Guinea-Bissau

2 Aprili 2010

Jamadari Indjai ndie mkuu mpya wa majeshi ?

https://p.dw.com/p/Mm4A
Bendera ya Guinea-Bissau yapepea upande gani ?

HALI YA KUTATANISHA

Kuna taarifa za kutatanisha kutoka Guinea-Bissau kuhusu iwapo waziri-mkuu Carlos Gomes Junior, ameachwa huru au bado yuko kizuizini nyumbani mwake. Mkuu mpya wa majeshi Jamadari Antonio Indjai,amearifu kwamba, nguvu zilizo oneshwa jana na wanajeshi walioasi, ni tatizo la ndani ya jeshi na na haina maana Jeshi, limenyakua madaraka. Jeshi, alisema mkuu huyo mpya wa majeshi, liko chini ya mamlaka ya kisiasa .

Duru ya habari Jeshini mjini Bissau, imearifu kuwa , waziri-mkuu Gomes, alitiwa nguvuni afisini mwake jana ,akachukuliwa Makao Makuu ya zamani ya kijeshi ,halafu akarejeshwa afisini mwake kabla kusindikizwa nyumbani kwake. Aliekuwa mkuu wa majeshi,Jamadari Jose Zamora Induta, pamoja na wanajeshi 40, walikamatwa -kwa muujibu wa duru jeshini. Wakaongozwa chini ya ulinzi mkali hadi kambi ya wanahewa karibu na uwanja wa ndege. Rais Malam Bacai Sanha ,wa Guinea-Bissau, ameungama kuwa Jamadari Induta, yumo kizuizini.

MKUU MPYA WA JESHI:

Mkuu mpya wa Jeshi ,Jamadari Indjai, ambae hapo kabla alikuwa makamo-mkuu wa Jeshi, amepewa sasa mamlaka ya kuidhibiti hali ya mambo nchini Guinea-Bissau.Matangazo ya radio ya taifa yalikatizwa kwa muziki wa kijeshi,lakini mamia ya waandamanaji , walijikusanya nje ya jumba la waziri mkuu wakilalamika kukamatwa kwake.

Jamadari Indjai, alitishia kumua waziri-mkuu Gomes ambae maarufu kwa jina la "Cadogo", ikiwa wafuasi wake wangeendelea kudai kuachiwa kwake. Ulipoingia usiku ,waandamanaji hao walitawanyika.

Wanajeshi wakionekana dhahiri kandoni mwa kambi za kijeshi huku mamia ya wananchi wajkijikusanya mbele ya makao makuu ya serikali huku wakipaza sauti: "Muacheni huru Cadogo na tumechoshwa na matumizi ya nguvu."

SAUTI ZA WALIMWENGU:

Ulimwenguni, sauti nyingi zimesikika zikilaani visa vilivyotokea jana Guinea-Bissau:kuanzia UM,Umoja wa Ulaya,Marekani na nchi mojawapo za ulaya:Katibu mkuu wa UM Ban Ki-moon, ameitisha suluhisho la amani la mzozo huu.Dola la zamani la kikoloni,Ureno,Marekani,Ufaransa na hata Umoja wa Afrika, zimeitaka Guinea-Bissau, kurejea katika utawala wa kikatiba.Msemaji wa siasa za nje wa UU Bibi Catherine Ashton,ametoa taarifa inayosema "Umoja wa Ulaya, unalaani kwa ukali kabisa hatua zilizochukuliwa na baadhi ya maafisa wa jeshi nchini Guinea-Bissau."

Guinea-Bissau, ilikumbwa pia na machafuko Machi, mwaka 2009 pale rais Joao Bernardo Vieira, alipouliwa na wanajeshi,pengine ili kulipiza kisasi kwa kuuwawa masaa machache kabla , kwa mkuu wa majeshi.Guinea-Bissau, ilinyakua uhuru wake kutoka Ureno, 1974.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Uhariri: Saumu Yusuf