Hali ya kisiasa Lebanon bado ya mvutano.
14 Februari 2008Mamia kwa maelfu ya wafuasi wa serikali nchini Lebanon walikusanyika leo katikati mwa mji mkuu Beirut kawa ajili ya kumbukumbu ya mwaka wa tatu tangu kuuwawa Waziri mkuu wa zamani Rafik Hariri, wakati maili kadhaa kutoka hapo, wakikusanyika wafuasi wa chama cha upinzani Hezbollah kwa mazishi ya kamanda wa ngazi ya juu aliyeuwawa jana katika mripuko wa bomu lilotegwa garini katika mji mkuu wa Syria-Damascus.
Wanajeshi na askari wa usalama waliwekwa kwa wingi katika mji huo mkuú, pakihofiwa uwezekano wa mapambano kati ya wafuasi wa pande hizo mbili. Katikati mwa Beirut mahala alipozikwa Hariri ,wafuasi wa serikali walikua na bebndeara na picha za kiongozi huyo pamoja na za wanasiasa wengine waliouwawa katika kipindi cha miaka mitatu iliopita. Jamaa wa marehemu Hariri na wanasiasa wa serikali ya muungano waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu.Pia lilizinduliwa sanamu la shaba linalofanana na mwenge likiawa na maandishi yenye kusifu mchango na kazi iliofanywa na hayati Hariri.
Wanasiasa walitoa hotuba kali wakitoa wito wa kumalizwa hali ya mkwamo iliosababishwa na mvutano unaoendelea kumpata rais mpya baada ya muda wa Rais wa zamani Emile Lahoud kumalizika mwezi Novemba mwaka jana na kuishutumu nchi jirani ya Syria kwa kujiingiza katika mambo ya ndani ya Lebanon.
Serikali ilitangaza leo kuwa siku ya mapumziko kumkumbuka waziri mkuu huyo wa zamani.
Kwa upande mwengine katika vitongoji vya washia kusini mwa Beirut, wafuasi wa chama cha msimamo mkali Hezbollah walikua wakiandaa mazishi ya mmoja kati ya makamanda wa ngazi ya juu Imad Mughnieh aliyeuwawa jana katika mji mkuu wa Syria Damascus katika mripuko wa bomu lililotegwa garini, ambapo Hebzbollah imeishutumu Israel shutuma amabazo zimepingwa na viongozi wa Israel, licha ya kusema kwamba pamoja na hayo inafurahia kuuwawa kwa Mughnieh aliyekua na umri wa miaka 45 wakisema ni ushindi katika vita dhidi ya ugaidi.
Maoni sawa na hayo yametolewa pia na wizara ya mambo aya nchi za nje ya Marekani iliyosema "dunia patakua mahala pema zaidi bila ya Mughnieh." ambaye amehusishwa na matukio kadhaa ya kigaidi dhidi ya Marekani ana Israel.
Akiwahutubia wafuasi wake kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliatangaza vita dhidi ya Israel akisema kama wazayuni wanataka vita basi watavipata.
Wakati huo huo Kiongozi mkuu nchini Iran Ayatollah Ali Khamenei alituma risala ya rambi rambi kwa Nasrallah akimtaja Mughnieh kuwa " Mtu jasiri."
Televisheni ya taifa mjini Teheran ikatangaza kwamba Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Manouchehr Mottaki atakwenda Lebanon kuhudhuria mazishi hayo, lakini haikuweza kufahamika kama amefanya safari hiyo au la. Iran sawa na ilivyo Syria ni waungaji mkono wakubwa wa Hezbollah na zote zimekua zikishutumiwa na wanasiasa wa msimamo wa wastani nchini Lebanon na pia nchi za magharibi, kuchangia katika kuitia msukosuko nchi hiyo.