1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kiongozi wa kijeshi wa Guinea ikoje ?

30 Desemba 2009

Kinyan'ganyiro cha madaraka chaendelea chini kwa chini ?

https://p.dw.com/p/LH3l

Kiongozi wa muda wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Guinea, Jamadari Sekouba Konate,jana alimtembelea Kiongozi wa Utawala wa Kijeshi wa nchi hiyo nchini Morocco na baadae akaarifu kuwa, Captain Moussa Camara, hatambui kinachopita pembezoni mwake.Hii ni kwa muujibu wa duru ya utawala huo wa kijeshi ilivyoliarifu shirika la habari la Ufaransa AFP.

Kuna taarifa pia za kutatanisha juu ya mpango wa kuwaacha huru hapo jana wanajeshi 15 ambao walitiwa nguvuni pale jeshi liliponyakua madaraka Desemba mwaka jana walipo tuhumiwa kuhatarisha usalama wa Taifa.

Jamadari Sekouba Konate, amemtembelea Captain camara kwa mara ya kwanza hapo jana hospitali nchini Morocco ambako anatibiwa baada ya kufyatuliwa risasi kichwani na mlinzi wake wa chanda na pete hapo Desemba 3, mwaka huu.

Baada ya matembezi hayo, Kiongozi huyo wa mpito hakusema chochote hadharani,lakini kwa muujibu wa duru za utawala wa kijeshi ,Jamadari Konate,anasemekana kusema kwamba Captain Dadis Camara ,hatambui kinachopita.

Anasemekana kuongeza kusema pia kwamba, hakuna tena la kufanya kwa Kiongozi huyo anaeugua.Hali ya afya ya Captain Camara, tangu kupigwa risasi kichwani imesababisha uvumi mwingi nchini Guinea-Conackry.Awali ,vyombo vya habari vya serikali nchini

vilitangaza kwamba Kiongozi huyo wa kijeshi anapata nafuu na atarejea nyumbani haraka kama iwezekanavyo.Captain Camara binafsi hakutoa taarifa yoyote hadharani au hatakujitokeza mbele ya watu tangu kushambuliwa.Isitoshe, Jamadari Konate, kiongozi wa mpito wa Guinea, aliahirisha mara kwa mara ziara yake nchini Morocco kumjulia hali Captain Camara.

Baada ya kushambuliwa Captain Camara, Jamadari Konate, ambae pia ni waziri wa ulinzi hivi sasa,alichukua dhamana ya uongozi wa Guinea,miezi 2 tangu wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji wa chama cha upinzani katika uwanja wa mpira na kuwaua watu kadhaa wake kwa waume .

Mashirika ya haki za binadamu yamedai kuwa, hadi wapinzani 150 waliuwawa na mamia kadhaa walijeruhiwa pamoja na wanawake wengi kubakwa uwanjani humo.

Captain Camara,anaeugua nchini Morocco, alinyakua madaraka Desemba 23, mwaka jana masaa tu , baada ya kuaga dunia kwa Rais Lansana Conte,jamadari wa zamani alieitwala Guinea, tangu 1984.

Taarifa za kutatanisha jana juu ya kuachwa huru au kutoachwa huru kwa kikundi cha wanajeshi 15 waliotiwa korokoroni kwa sababu za usalama,zinabainisha kinyan'ganyiro cha madaraka kinachoendelea miongoni mwa vikundi mbali mbali ndani ya utawala wa kijeshi wa Guinea.

Mwandishi: Ramadhan Ali / AFPE

Uhariri: Othman Miraji