1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya kibinaadamu Ukraine ni mbaya

6 Agosti 2014

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amelionya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mkutano wa dharura Jumanne(05.08.2014) kwamba hali ya kibinaadamu mashariki mwa Ukraine inazidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/1CpWV
Wakaazi waliokimbilia kwenye kituo cha kujihifadhi na mashambulizi ya mabomu huko Gorlovka, Donetsk .(o5.08.2014)
Wakaazi waliokimbilia kwenye kituo cha kujihifadhi na mashambulizi ya mabomu huko Gorlovka, Donetsk .(o5.08.2014)Picha: picture-alliance/dpa

John Ging mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu operesheni za kibinaadamu (OCHA) akizungumza katika kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makao makuu ya Umoja huo mjini New York amesema "Watu wanaokadiriwa kufikia milioni 3.9 wanaishi katika maeneo yalioathirika moja kwa moja na ghasia hizo .Wale waliobakia kwenye kanda za mzozo wanakabiliwa na tishio la usalama kutokana na mapigano ambayo yanazidi kutokea katika maeneo ya mijini yenye wakaazi wengi."

Amesema mapigano hayo yamesababisha uharibifu mkubwa kwa miundo mbinu na kuathiri huduma za umeme na maji na upatikanaji wa huduma nyengine za msingi ambapo pia nyumba zimekuwa zikiangamizwa na wafanyakazi wa huduma za matibabu wamekuwa wakikimbia kuhami kunusuru maisha yao.

Ameongeza kusema kwamba ghasia hususan katika maeneo ya mijini zitawatumbukiza hatarini watu wengi zaidi na kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wanaouwawa iwapo ufumbuzi wa kisiasa katika mzozo huo utashindwa kupatikana.

Mkutano huo uliombwa na Urusi baada ya mapigano mashariki mwa Ukraine kuingia katika ngome kuu ya waasi kwenye mji wa Donetsk.Waasi wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi hapo jana wameshambuliana kwa maroketi katika mapambano mapya tokea pande hizo mbili zianze kupigana hapo mwezi wa Aprili.

John Ging Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu operesheni za kibinaadamu (OCHA) .
John Ging Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloratibu operesheni za kibinaadamu (OCHA) .Picha: picture-alliance/AA

Mkono wa Urusi katika mzozo

Ukraine na mataifa ya magharibi yamekuwa yakiishutumu Urusi kwa kuchochea uasi huo kwa kuwapatia waasi silaha na wanajeshi madai ambayo serikali ya Urusi imekuwa ikiyakanusha mara kwa mara.

Imeripotiwa kuwa zaidi ya watu 4,000 wamejeruhiwa mashariki ya Ukraine tokea mwezi wa Aprili.Takriban wengine 58,000 wameondoka tokea mapema mwezi wa Julai na wengine zaidi ya 1,000 wanakimbia kila siku.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin.
Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin.Picha: picture-alliance/dpa

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin amesema hali mashariki ya Ukraine hususan katika miji ya Luhansk na Donetsk ni ya maafa. Amelishutumu jeshi la Ukraine kwa kuzishambulia ovyo nyumba kwa mabomu ambapo amesema katika miji midogo asilimia 80 ya nyumba zimeharibiwa na mamia ya majengo yameanguka.

Amesema "Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limetambuwa rasmi kwamba kuna mzozo wa ndani unaohusisha matumizi ya silaha mashariki ya Ukraine.Licha ya makubaliano ya kimataifa yakiwemo yale yaliofikiwa Geneva na Berlin yaliosainiwa na serikali ya Ukraine, serikali ya nchi hiyo inazidi kuimarisha operesheni zake za kijeshi na kusababisha mauaji ya mamia ya watu."

Kituko cha Urusi

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo amehoji iwapo suala hilo la hali ya kibinaadamu nchini Ukraine lilistahiki kuitishiwa mkutano huo wa dharura maoni ambayo yameungwa mkono na Rwanda.

Mizinga ya vikosi vya Ukraine iliowekwa nje ya Siversk, Donetsk .
Mizinga ya vikosi vya Ukraine iliowekwa nje ya Siversk, Donetsk .Picha: picture-alliance/AP Photo

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Mark Lyall Grant amesema ni kituko kikubwa kwa Urusi kuitisha mkutano huo wa dharura wa baraza la usalama kujadili maafa ya kibinaadamu ambayo kwa kiasi kikubwa imeyasababisha yenyewe.

Mapigano mashariki ya Ukraine yamewalazimisha zaidi ya watu 285,000 kukimbia makaazi yao.Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema zaidi ya watu 117,000 wamekimbilia maeneo mengine ndani ya nchi hiyo wakati wengine 168,000 wamevuka mpaka na kuingia Urusi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters

Mhariri : Iddi Ssessanga