Hali ya hewa na sekta ya uchumi
6 Desemba 2005Ukiangalia idadi hizi ni rahisi kufahamu kwamba ili kuyalinda mazingira lazima sekta ya uchumi ihusishwe, kama anavyosema Axel Michaelowa, mtafiti wa hali ya hewa kutoka taasisi ya uchumi wa kimataifa mjini Hamburg, Ujerumani: “Gesi ya Carbon Dioxide ambayo inaongeza ujoto angani hutolewa kupitia kila shughuli ya uchumi, kama ni viwanda, malori au ndege. Kampuni zinazotoa zaidi gesi hii ni viwanda vya kutengeneza vyuma vya pua na nishati. Kutokana na sheria maalum ya Umoja wa Ulaya kampuni hizi zinalazimishwa kununua leseni kwa kutoa Carbon Dioxide, kwa hivyo inabidi zifikirie njia za kupunguza utoaji wao.”
Hata kampuni kubwa kabisa duniani, Generel Electric la Marekani, lilibadilisha msimamo wao. Mkurugenzi wa shirika hilo alisema na ninamnukuu: “Tunaona tishio la hali ya hewa. Na tunajua: Sasa ni wakati wa kuanza kuchukua hatia!”- mwisho wa kumnukuu. Mwenendo mwingine ni kwamba masoko ya kifedha ya kimataifa yanaangalia kwa uangalifu matokeo kuhusu hali ya hewa. Kwa mujibu wa Axel Michaelowa haiwezekani kutegemea soko huru ili kupunguza utoaji wa gesi chafu lakini lazima serikali ziweke sheria. Katika nchi za Ujerumani na Japan kampuni kadhaa ziliwahi kujitolea kupunguza utoaji wao wa gesi ya Carbon Dioxide lakini nyingine hazijachukua hatua yoyote.
Bado kuna muda mrefu kabla athari zitakazosababisha mabadiliko ya hali ya hewa kujitokeza na sekta ya uchumi haiwezi kupanga vitega uchumi. Kwa hiyo makampuni yanasubiri masharti ya serikali. Lazima mkutano wa Montreal uweke msingi, anasema Axel Michaelowa kutoka Hamburg: “Bila shaka! Mada kuu hapa Montreal ni vipi tutakavyoendelea mbele wakati makubaliano ya Kyoto yatakapomalizika mwaka 2012. Afadhali tuwe na mpango kwa miaka 10 au 15 ijayo kwa sababu sehemu kubwa ya vitega uchumi inalenga kipindi cha miaka 10 au hata 30. Kwa hivyo inabidi tuweke ishara hapa Montreal kwamba tunakubali kuendelea kuilinda hali ya hewa hata baada ya mwaka 2012.”
Kulinda hali ya hewa inapanua soko la kibiashara. Shirika la kimataifa la nishati linatarajia kiasi cha vitega uchumi katika sekta ya nishati kufikia dola za Kimarekani trilioni 16 katika muda wa miaka 25 ijayo. Mtaalamu wa Ujerumani Bwana Michaelowa analinganisha soko la nishati na sekta ya mtandao wa Internet iliyostawi ghafla. Kila mahali kuna kampuni ndogondogo zilizotengeneza teknolojia maalum ya kupunguza utoaji wa gesi chafu. Mashirika haya yanaweza kunufaika pia kutokana na ushirikiano na nchi zinazoendelea ambazo zinahitaji sana teknolojia hiyo katika kujiendeleza kiuchumi bila ya kuyaharibu mazingira.