1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya hewa Brazil mpinzani mwenye nguvu?

25 Mei 2014

Wakati mashindano ya Kombe la Soka la Dunia yakikaribia kuanza, hali ya hewa nchini Brazil inatajwa kuwa changamoto kubwa kwa wachezaji wa kombe hilo maarufu zaidi ulimwenguni kutoka Ujerumani

https://p.dw.com/p/1C3bh
Brasilien Fortaleza
Picha: picture-alliance/dpa

Na sasa swali ni kuwa msakata kabumbu atapaswa kupambana na vingapi awapo uwanjani kabla ya timu yake haijaibuka na ushindi.

Hata kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, hali ya hewa ya Brazil imeshalifunika kombe lenyewe. Ni vipi, timu kama ya Ujerumani inaweza kushinda mechi zinazochezwa chini ya mionzi mikali ya jua la tropiki? Ureno, Ghana na Marekani ni timu zinazofahamika kuwa kwenye kundi moja ya Ujerumani. Lakini badala ya mabingwa wa dunia wa soka Cristiano Ronaldo na Kevin-Prince Boateng, kikwazo kikubwa kwa wachezaji wa timu ya soka ya Ujerumani ni hali ya hewa. Mechi ambazo Ujerumani itacheza mjini Salvador, mnamo tarehe 16 Juni, Fortaleza, tarehe 21 na Recife ya tarehe 26 Juni, zitachezwa huku nyuzijoto zikiwa ni 30, saa saba adhuhuri hadi 10 alasiri, katikati ya joto la Brazil.

Mji wa Fortaleza, kwa mfano, uko kwenye mstari wa Ikweta kabisa, na sio kabisa hata hali ya hewa ya kitropiki ambayo wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani angalau wangelikuwa wanaiota. Na miji ya Recife na Salvador, sio tu kwamba ina joto kali bali pia ina unyevuunyevu wa kiwango cha juu katika mwezi Juni, unaofikia hadi asilimia 85. Kwa Ujerumani, hata unyevuunyevu ukiwa kwa asilimia 20 huwa tayari unachukuliwa ni kiwango kisichopendeza wakati wa majira ya kiangazi.

Brasilien Joachim Löw Costa do Sauipe Strand
Picha: picture-alliance/dpa

“Unapokuwa hujazowea mazingira ya joto, unakuwa na kiwango kidogo cha ufanisi,” anasema Mark de Marees, daktari kwenye Kitivo cha Sayansi ya Michezo katika Chuo Kikuu cha Cologne, akisisitiza kuwa joto lina athari ya moja kwa moja kwa ufanyajikazi wa kiwiliwili. Na kwa hilo, daktari huyo anawapa ushauri wachezaji wa Ujerumani kujiandaa na mapema na hali hiyo.

Utafiti unaonesha kuwa inachukua kiasi cha siku kumi kwa mwili kuweza kuzoea hali ya hewa, na hivyo ushauri ni kuwa timu ya taifa ya Ujerumani iwasili Brazil angalau siku kumi kabla ya michuano kuanza. Kwa maneno ya daktari huyo, mwili unaanza kuzoea joto kwa viwango tafauti, kwa kuanza na kutoka jasho ili kuweka sawa jotoridi la mwili na kisha jasho la kuimarisha mwili. Na hilo linajumuisha pia na kutumia madini ambayo yanausaidia mwili kualakiana na mazingira kirahisi na pasipo madhara.

Ili mwili huo uweze kufika kiwango cha kufanya kazi inavyotakiwa katika mazingira ya joto kali ambayo haukuyazoea, ni lazima mfumo wa usukumaji damu na usambazaji hewa uwe makini. Vyenginevyo, unaweza kufeli kwa ghafla na kusababisha hasara na madhara.

Uwanja wa Recife Arena Pernambuco ambao Ujerumani itacheza baadhi ya mechi zake
Uwanja wa Recife Arena Pernambuco ambao Ujerumani itacheza baadhi ya mechi zakePicha: Getty Images/AFP

Eneo la Manaus lililo kaskazinik mashariki mwa Brazil linachukuwa sehemu muafaka kabisa. Likiwa kwenye milima ya Amazon, linapata misimu ya mvua kali na kiangazi. Huko joto si jambo kubwa sana, ingawa huwa kukavu wakati wa kile kinachoitwa kipupwe cha Brazil.

Kwa mujibu wa Profesa Hans-Joachim Appell Coriolano anayeusika na elimu ya mifupa na upasuaji kwenye Chuo Kikuu cha Cologne, kila mtu anapokuwa kwenye sehemu yenye hewa ya kutosha, basi anapunguza uwezekano wa kukabiliwa na matatizo yatokanayo na joto hata kama si mazingira aliyoyazowea. Lakini bado, upoteaji wa maji na madini mengi wakati wa michezo katikati ya joto la Brazil, lazima ufidiwe kwa wachezaji kunywa maji mengi sana, anasema profesa huyo.

Kwa vyovyote vile, mabadiliko ya hali ya hewa ni mtihani mkubwa kwa wachezaji wa Ujerumani, na kocha wao, Jochim Löw analifahamu hilo. Ndio maana anapozungumzia wasifu wa mchezaji wake kwenye Kombe hili anataja sifa ya kuwa ni yule mtu anayeweza kualakiana na hali ya hewa mpya. “Hapana shaka, ni vigumu kupata kikosi ambacho kitakabiliana na hali ilivyo, maana kucheza mara tatu kwenye joto la kiasi hicho kunahitaji zaidi ya ujasiri,” anasema Löw.

Mwandishi: Jessica Balleer
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Yusuf Saumu