1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya Hatari yatangazwa Tripoli, Libya

Caro Robi
3 Septemba 2018

Hali ya hatari imetangazwa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli na maeneo yaliyo karibu kufuatia mapigano makali kati ya makundi hasimu ya wapiganaji ambayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 39 na wengine kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/34CLM
Libyen Bürgerkrieg
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. Messara

Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa yenye makao yake mjini Tripoli, imetangaza kuwa kutokana na hatari iliyopo kufuatia mapigano hayo na kuzingatia na maslahi ya umma, inatangaza hali ya hatari katika mji mkuu na viunga vyake ili kuwalinda raia, mali pamoja na asasi muhimu.

Serikali hiyo ya Libya imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kuheshimiwa kwa makubaliano ya kusitisha uhasama.

Hayo yanakuja huku takriban wafungwa 400 wakitoroka kutoka jela moja kusini mwa Tripoli, eneo ambalo pia limeshuhudia mapigano makali katika kipindi cha juma moja lililopita kati ya makundi mawili hasimu ya wapiganaji.

Wafungwa hao walifungua milango ya jela ya Ain Zara na askari walishindwa kuwazuia. Umoja wa Mataifa umezitaka pande zinazozana kufanya mkutano wa dharura kesho Jumanne kujaribu kujadili hali hiyo mbaya ya kiusalama na kutafuta njia za kumaliza mapigano.

Umoja wa Mataifa wataka pande zinazozana kukutana

Makabiliano makali yalizuka wiki iliyopita kati ya kundi lijulikanalo kikosi cha Saba au kwa jina jingine Kaniyat linalotokea Tarhouna kilomita 65 kusini mashariki mwa Tripoli dhidi ya makundi ya Tripoli Revolutionaries TRB na Nawasi ambayo ni makundi makubwa zaidi ya wapiganaji mjini humo.

Libyen Tripolis Kämpfe zwischen Milizen
Moshi waonekana ukifuka Tripoli, Libya wakati wa mapiganoPicha: Reuters/H. Amara

Libya inaongozwa na serikali mbili moja ikiwa na makao yake mjini Tripoli na nyingine isiyotambuliwa na jumuiya ya kimataifa ikiwa na makao yake mjini Tibrouk.

Licha ya kuwa serikali ya Tripoli ndiyo inayotambuliwa kimataifa, haina udhibiti wa mji mkuu ambako makundi ya wapiganaji yanaoiunga mkono wanaendesha operesheni zao kwa uhuru, mara nyingi wakiwa na uchu wa kupata fedha na madaraka.

Kwingineko, kombora lilianguka katika kambi inayowahifadhi watu wa kabila la Tawergha walioyakimbia makazi yao ya Al Fallah, na kuwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine saba wakiwemo watoto wawili.

Jamii ya Tawergha walilazimika kuyahama makazi yao karibu na mji wa Misrata wakati wa operesheni iliyoendeshwa na jumuiya ya kujihamii ya NATO ya kumng'oa madarakani aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011 na watu wa kabila hilo wamezuiwa tangu wakati huo kurejea katika makazi yao.

Libya, taifa la kaskazini mwa Afrika limekumbwa na msukosuko tangu kuondolewa na hatimaye kuuawa kwa Gaddafi mwaka 2011, huku makundi ya waasi yakipambana mara kwa mara, kumeibuka makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali na kusababisha taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kushindwa kutawalika.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri: Gakuba, Daniel