Hali ni shwari Uingereza baada ya polisi kumwagwa
11 Agosti 2011Kuwapo na polisi wengi zaidi katika miji mikubwa ya Uingereza hadi sasa kumezuwia usiku wa tano wa ghasia, kukiwa hakuna ripoti za ghasia kubwa. Mapema jana , waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameahidi kumaliza kile alichokiita ghasia za kuchukiza nchini humo. Amesema kuwa iwapo ghasia zitaendelea, polisi huenda wakaamua kutumia silaha ya mabomba ya maji kwa mara ya kwanza nchini Uingereza. Maafisa 16,000 wa polisi wamewekwa katika mji wa London kwa usiku wa pili hii leo. Miji mingine kaskazini na kati ya Uingereza kama Manchester, Liverpool na Birmingham, ambayo imeshuhudia ghasia mbaya zaidi siku ya Jumanne usiku, pia inaonekana kuwa shwari. Zaidi ya watu 1,000 wamekamatwa, ambapo watu 805 wamekamatwa mjini London pekee. Katika ishara ya kuchukua hatua za haraka za kisheria, maafisa mjini Manchester wametoa hukumu na watu wawili wamehukumiwa kifungo.