1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Libya

8 Agosti 2011

Waasi wa Libya wanaosemekana kuudhibiti mji wa Bir al Ghanam,umbali wa kilomita 80 kusini mwa mji mkuu Tripoli wameelezea azma ya kusonga mbele kuelekea mji mkuu huo- ngome ya kanali Muammar Gaddafi.

https://p.dw.com/p/12D4n
Mizinga inaripuliwa mjini TripoliPicha: dapd

Mji huo mdogo wa jangwani ni kituo cha karibu zaidi na mji mkuu wa Libya Tripoli ambacho waasi wamefanikiwa kukiteka hadi wakati huu.Wanamgambo wanaopigana dhidi ya serikali ya kanali Muammar Gaddafi walipiga kambi pembezoni mwa Bir al Ghanam tangu mwishoni mwa mwezi wa June bila ya kuweza kusonga mbele.

Wameliambia shirika la habari la Reuters hii leo wameshaingia ndani ya mji huo tangu jumamosi iliyopita wakisaidiwa na madege ya kivita ya jumuia ya kujihami ya NATO.

Wanasema kituo wanachokilenga hivi sasa ni Zaouia,mji wa mwambao ulioko umbali wa kilomita 50 magharibi ya mji mkuu-Tripoli.

Libyen / Gaddafi / Tripolis
Muammar GaddafiPicha: AP

Waziri mkuu wa Libya Al Baghdadi Ali al Mahmoudi amesema hata hivyo vikosi vya serikali vimeukomboa mji wa Bir Ghanam baada ya kuwarejesha nyuma waasi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza Reuters, katika mji huo wa jangwani-Bir-Ghanam,hakuna mwanajeshi yoyote wa serikali ya Gaddafi aliyeonekana.Badala yake wanasema wamegundua vifaru vitatu vilivyotiwa moto na bunduki moja iliyotupwa.

Waasi na washirika wao wa NATO wanataraji huenda wakanyakuwa madaraka pindi wakizidi kumtia kishindo,,kuwahujumu wanajeshi wake,kumkosesha silaha,mafuta na kumzuwilia fedha.

Wadadisi wanahisi hata hivyo pindi opereshini za NATO zikipungua,Muammar Gaddafi ataweza kupata njia ya kusalia madarakani. Baadhi ya wanachama wa NATO wameingiwa na hofu kutokana na kuendelea opereshini za madage ya kivita ya NATO dhidi ya Libya katika wakati huu wa shida za kiuchumi.Hata hivyo hakuna dalili ya kupungua opereshini hizo.

Libyen Rebellen Tripolis Gaddafi Kämpfe 01.08.2011
Waasi wanapumzika baada ya mapiganoPicha: AP

Jumuia ya kujihami ya NATO inasema hujuma za madege yake zimelengwa kuwalinda raia dhidi ya wanajeshi wa Gaddafi.Lakini kuna mambo tofauti yanayoonyesha NATO inaandaa opereshini zake kwa ushirikiano pamoja na waasi.

Jana helikopta za kivita za Uingereza Apache ziliruka toka manuari ya kivita iliyoko katika bahari ya Mediterenia na kutupa mizinga dhidi ya magari ya kijeshi huko Al Watyah-kituo cha kijeshi cha serikali kilichoko umbali wa kilomita 170 kusini magharibi ya Tripoli.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed