Hali bado yatisha Sudan Kusini
28 Aprili 2014Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya haki za Binadamu Navi Pillay yuko Sudan Kusini wakati ambapo nchi hiyo inazidi kukabiliwa na wimbi la mauaji huku sauti za kushutumu mauaji hayo zikiongezeka kusikika kutoka pembe zote za dunia.Navi Pillay pamoja na mjumbe maalum anayehusika na harakati za kuzuia maangamizi ya halaiki Adama Dieng waliwasili Juba mji mkuu wa Sudan Kusini hii leo.
Akitowa maelezo juu ya ratiba ya ziara ya wajumbe hao msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Joe Contreras amesema kwamba wanatarajiwa kubakia Sudan Kusini hadi siku ya Jumatano(30.04.2014) ambapo watakuwa na vikao na reais Salva kiir pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu nchin humo.Halikadhalika watatembelea maeneo yalikofanyika mauaji ya watu wengi endapo hali ya usalama itaruhusu.
Wiki iliyopita baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitowa kitisho cha kuweka vikwazo dhidi ya makundi yote yaliyoko vitani katika mgogoro huo wa Sudan Kusini,yaani vikosi vya serikali vinavyomuunga mkono rais Kiir na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar.Pande zote mbili zinahusishwa na kna mauaji ya kinyama pamoja na uhalifu wa kivita ikiwemo mauaji ya watu wengi,ubakaji,pamoja na kuzishambulia kambi za Umoja wa Mataifa zinazowahifadhi raia waliokimbia vita vya kikabila.
Aidha makundi hayo yanatajwa pia kuwaandikisha watoto katika makundi ya wapiganaji.Ziara ya Navi Pillay imekuja katika wakati ambapo kwenye nchi jirani ya Ethiopia mazungumzo ya amani kati ya serikali na waasi yalipangwa kufanyika hii leo kama walivyodokeza hapo awali wasuluhishi kutoka kanda hiyo ingawa inafahamika kwamba duru zilizopita za mazungumzo hayo hazikufanikiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mgogoro huo huku matumani ya kupigwa hatua yakionekana kuwa kidogo.
Kutoka na hali ilivyo ndani ya Sudan Kusini kwa hivi sasa sauti zimesikika pia za kutoa mwito wa kukutanishwa uso kwa macho mahasimu wawili,Kiir na Machar.Leo wajumbe wa Kimataifa waliokutana na Machar wiki iliyopita wametowa wito huo kupitia mjumbe wa Umoja wa Ulaya aliyekuweko pia katika ujumbe huo,Alexander Rondos.Rondos amesema mazungumzo ya ana kwa ana kati ya mahasimu hao wawili wa kisiasa ni hatua muhimu itakayomaliza harakati za kulipiziana kisasi na mauaji ambayo yamesababisha kuvunjika kabisa kwa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa Januari.
Mapema mwezi huu waasi walibebeshwa lawama ya kuhusika na mauaji ya mamia ya watu katika jimbo ambalo ni kitovu cha utajiri mkubwa wa mafuta nchini humo la Bentiu huku watu wanaounga mkono serikali wakijitokeza kwa upande mwingine na kuua raia kadhaa katika mashambulizi dhidi ya kambi ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Bor.
Hata hivyo kiongozi wa ujumbe wa serikali katika kundi la upatanishi ambaye ni waziri wa habari Michael Mauei pia alithibitisha kwamba huenda kukawepo uwezekano wa mazungumzo kuanza tena baadae leo.Wakati mazungumzo hayo yakiwekewa matumaini madogo hali ya mambo katika Sudan Kusini inazidi kuzorota,leo hii shirika la madaktari wasiojali mipaka MSF limetowa ushahidi mpya wa hali ilivyokuwa katika mauaji ya Bentiu.
Mkuu wa MSF nchini Sudan Kusini Raphael Gorgeu anasema alichokiona Bentiu ni miili ya watu iliyotapakaa kila mahala katika barabara za jimbo hilo mingine ikiliwa na mbwa na kudonolewa na ndege jambo ambalo amelitaja kama kitendo cha kutoweka ubinadamu.Wameshuhudia vile vile watu wakiuwawa katika hospitali kadhaa walizokuwa wamekimbilia baada ya hospitali hizo kushambuliwa.
Vita vya miezi minne Sudan Kusini vimesababisha maelfu kuuwawa na idadi hiyo huenda ikageuka na kuwa mamia kwa maelfu huku wengine zaidi ya milioni moja wakiwa wameitoroka nchi hiyo.Kuna zaidi ya raia 78,000 kwahivi sasa waliosongamana katika kambi nane za Umoja wa Mataifa nchini humo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman