1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado tete mjini Khartoum: Waandamanaji wasalia mtaani

Sylvia Mwehozi
26 Oktoba 2021

Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wameendelea kuzuia baadhi ya barabara na kuchoma matairi, huku maduka na huduma ya intaneti na mawasiliano ya simu vyote vikitatizika leo Jumanne. 

https://p.dw.com/p/42BgE
Sudan | Proteste in Khartoum
Picha: AFP/Getty Images

Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wamesalia katika mitaa ya Khartoum asubuhi ya leo na mji pacha wa Omdurman, huku barabara nyingi zikiwekwa vizuizi na matairi yaliyochomwa. Maduka yamefungwa, mawasiliano ya simu na huduma za intaneti navyo pia vimeendelea kuzuiwa huku watu wakipanga foleni kwa ajili ya kununua mkate, siku moja baada ya jeshi kudhibiti madaraka katika mapinduzi yaliyochochea vurugu ambapo watu saba wanadaiwa kupoteza maisha.Yanayoendelea Sudan: Jeshi lavunja serikali ya mpito

"Hali ya sasa ya Sudan ni mbaya lakini hatutakubali mapinduzi yoyote ya kijeshi katika nchi hii. Inatosha, miaka 30 ya udhalilishaji wa al-Bashir, hatutaki mapinduzi mengine sasa. Tunataka serikali ya kiraia iliyochaguliwa, watu hawa walioigeuka serikali wanataka kuwakilishwa kwa damu yao isiyo na hatia. Fedheha ambayo tumepitia inatosha," alisema mwandamanaji mmoja.

Waziri Mkuu Hamdok na viongozi wengine waandamizi wa serikali ya mpito ambao walikamatwa jana Jumatatu na jeshi bado wako kizuizini katika eneo lisilojulikana ingawa taarifa nyingine zinasema wanashikiliwa katika kambi moja ya kijeshi nje kidogo ya mji mkuu wa Khartoum.

Sudan General Abdel Fattah al-Burhan
Jenerali Abdel Fattah al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj /AA/picture alliance

Vikosi kutoka jeshi la Sudan na vile vya kikosi kinachohofiwa cha msaada wa haraka, vimepiga doria mjini Khartoum usiku mzima wa kuamkia leo na kujaribu kutawanya waandamanaji. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Human Rights Watch limedai kwamba vikosi hivyo vilitumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.

Wakati huohuo madaktari na watumishi wa umma nchini humo wameitisha mgomo mkuu kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyoondoa serikali ya kiraia jana Jumatatu. Tume kuu ya Madaktari wa Sudan imesema kuwa watagoma kutoa huduma katika hospitali zote nchini na zile za kijeshi isipokuwa tu watawahudumia wagonjwa wa dharura. Watumishi katika wizara, sekta ya umma na benki kuu nao pia wametangaza kujiunga na mgomo huo.

Mataifa ya magharibi yameendelea kulaani mapinduzi hayo na kutaka kuachiwa kwa waziri Mkuu Hamdok na maafisa wengine. Utawala wa Rais wa Marekni Joe Biden umetangaza kusitisha msaada wa dharura wa Dola milioni 700 kwa Sudan. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ametoa wito wa kukomeshwa vurugu dhidi ya waandamanaji na kurejeshwa kwa huduma ya intaneti. Amesema Marekani iko katika mazungumzo na washirika wake wa kuchukua mwelekeo wa pamoja wa kidiplomasia kushughulikia hali hiyo na pia kuzuia kukosekana kwa utulivu zaidi nchini Sudan na katika ukanda mzima.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kufanya mkutano wa dharura baadae leo kuzungumza mapinduzi hayo ya kijeshi. Kulingana na tathmini ya Umoja wa Mataifa, jeshi linaonekana kuchukua udhibiti wa mji mkuu Khartoum, huku uwanja wa ndege, madaraja na Televisheni ya taifa vikiwa chini ya vikosi vya usalama na eneo la kuingia katika mji huo pia limezuiwa.