1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni tete Guinea

17 Novemba 2010

Waziri Mkuu wa serikali ya mpito nchini Guinea, Jean Marie Dore, amewaita wafuasi wa mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais, Cellou Dalen Diallo, kuwa ni wahuni.

https://p.dw.com/p/QBP3
Polisi wakiwa silaha nje ya Conakry.Picha: AP

Wafuasi hao wamekuwa wakifanya ghasia kupinga ushindi wa Alpha Conde.

Akizungumza katika televisheni ya taifa, Waziri Mkuu huyo wa mpito, Jean Marie Dore, amesema katika siku za hivi karibuni, wahuni wamekuwa wakijiingiza katika ghasia kwa kuwalenga wananchi wasiyo na hatia pamoja na mali zao.

Amesema kisingizo cha ghasia na vurugu hizo ni tangazo la matokeo hapo siku ya Jumatatu, ambayo yalionesha kuwa Bwana Conde ameshinda katika uchaguzi wa urais, ambapo mpinzani wake mkuu, Cellou Dalen Diallo, alipinga, akisema kulifanyika wizi wa kura. Alpha Conde kutoka upande wa upinzani ametangazwa mshindi kwa asilimia 52.52, huku mpizani wake, Diallo, akipata asilimia 47.48.

Diallo ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani amekata rufaa katika  mahakama kuu ya nchi hiyo ambayo, kwa mujibu wa sheria, ni lazima ithibitishe na kuyaridhia matokeo hayo kabla ya kuapishwa kwa mshindi.

Guinea Alpha Conde Wahlen
Alpha Conde akizungukwa na kushagiliwa na wafuasi wakePicha: AP

Hapo jana wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Waislam ya Eid al-Adha, Bwana Conde alivinjari mitaani kwenye maeneo matatu nje ya mji mkuu Conakry alikopata kura nyingi kuwashukuru wananchi.

Hotuba hiyo ya Waziri Mkuu wa mpito imetolewa huku hali ya wasi wasi wa kuzuka mapigano ya kikabila ikizidi kuongezeka. Watu wa kabila la Fulani analotoka Cellou Dalen Diallo na kabila la Malinke analotoka  Alpha Conde.

Kwa upande mwengine, idadi ya watu waliokufa kutokana na ghasia hizo imezidi kuongezeka, baada ya hii leo maiti tatu kupatikana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Conakry.

Amara Camara,  ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini humo, amethibitisha kwamba miili hiyo imepatikana katika maeneo tofauti, huko Ratoma ambalo ni eneo pekee Bwana Diallo alikopata kura nyingi.

Katika mkoa wa Kanema, polisi wamesema watu kiasi ya 20 wamekamatwa kutokana na vitendo vya uporaji wakati wa ghasia kati ya watu wa kabila la Malinke na Peul, makabila ambayo ni hasimu kwenye eneo hilo.Hii ni kutokana na matokeo hayo ya uchaguzi wa urais.

Kanema ni eneo lililoko kwenye mpaka wa Guinea na nchi za Liberia na Sierra Leone ambazo zinarejea kwenye hali ya kawaida kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Na wafuatiliaji wa siasa za Guinea wanahofu kuwa hali hiyo ya kuibuka kwa mapigano ya kikabila huko Guinea isipodhibitiwa, huenda ikasambaa na kuziathiri nchi hizo jirani na Guinea.

Mjini Washington, Marekani imetoa wito wa kurejeshwa kwa hali ya usalama na utulivu nchini Guinea. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Phillip Crowley, amewataka  Bwana Conde na Bwana Diallo kuwaomba wafuasi wao watulie ili kutoa nafasi kwa mahakama kuu kuchunguza iwapo kulikuwepo na hila zozote kwenye uchaguzi huo.

Iwapo mahakama hiyo itayathibitisha matokeo hayo, Bwana Conde atakuwa rais wa nne wa Guinea tokea ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka 1958.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Othman Miraji