Hakuna uchaguzi DRC hadi katikati mwa 2019, yasema tume
11 Oktoba 2017Awali uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika Novemba 2016. Kalenda iliyotangazwa na tume ya uchaguzi inakiuka makubaliano yaliofikiwa kati ya Kabila na wawakilishi wa upande wa upinzani, kwamba uchaguzi ungefanyika kabla ya mwishoni mwa mwaka huu.
Dazen kadhaa za watu waliuawa mwaka 2016 katika maandamano dhidi ya hatua ya Kabila kukataa kuachia madaraka baada ya kumalizika kwa muhula wake anaoruhusiwa kikatiba. Baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yako mikononi mwa waasi wanaosema hawatasitisha mapigano wakati Kabila akiendelea kuwepo madarakani.
Tume ya uchaguzi wa DRC CENI ilisema katika taarifa kufutia mkutano na wawakilishi wa mashirika ya kiraia siku ya Jumanne, kwamba itahitaji alau siku 504 kuandaa uchaguzi baada ya kukamilika kwa zoezi la kuandikisha wapigakura.
Uandikishaji ulianza katika badhi ya maeneo ya mkoa uliokumbwa na machafuko wa Kasai katikati mwa mwezi Septemba, na tume ilisema kimsingi zoezi hilo litachukuwa karibu miezi mitatu. Hilo lina maana kwamba kura haiwezi kuitishwa hadi Aprili 2019.
Upinzani unamtuhumu Kabila kwa kujairbu kung'ang'ania madarakani kwa kuahirisha uchaguzi hadi atakapopata njia ya kuondoa ukomo wa mihula inayomzuwia kugombea kwa mara nyingine, kama walivyofanya wenzake katika mataifa ya Rwanda na Jamhuri ya Congo.
'Hakuna majadiliano tena na Kabila'
Mwenyekit wa Tume hiyo, Corneille Nangaa, hajatangaza rasmi kalenda ya uchaguzi lakini ameendesha kampeni ya kuwahamasisha viongozi wa kidini na wale wa mashirika ya kiraia. Pendekezo hilo tayari limezua ukosoaji mkali kutoka upinzani, ambao umelezea kwamba tume huru ya uchaguzi imekuwa ikitekeleza ajenda ya Rais kabila na chama chake.
"Hakuna tena uwezekano wa mazungumzo na Bwana Kabila kwa sababu hana nia ya kuachia madaraka…tunachosubiri sasa ni kuwepo na uchaguzi kabla ya Desemba 31 mwaka huu. Ikiwa hakutokueko na uchaguzi, basi ni lazima kuweko na kipindi cha mpito ambacho rais wa sasa hatoshiriki tena. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, linatakiwa kubeba dahamana yake ili kuwepo na suluhisho la haraka nchini Kongo," alisema mbunge Martin Fayulu, kiongozi wa chama cha upinzani cha ECiDE.
Kabila ambaye alichukuwa madaraka baada ya kuuawa kwa baba yake Laurent kabila mwaka 2001, anakanusha kwamba ana nia ya kusalia madarakani, na anasema kucheleweshwa kwa uchaguzi kunatokana na ugumu katika kuandikisha mamilioni ya wapigakura na kutafuta mamilioni ya dola zinazohitajika kufadhili uchaguzihuo.
Congo haijawahi kushuhudia mabadiliko ya amani ya uongozi na kukataa kwa Kabila kuka pembeni mwaka uliopita, kumechochea hali ya ukosefu wa usalama nchini humo, ambako mamilioni walikufa katika migogoro ya kikanda kati ya 1996-2003, wengi wao kutokana na njaa na magonjwa.
Uasi uliozuka katika mkoa wa Kasai umesababisha vifo vya hadi watu 5,000 na kuwafanya wengine milioni 1.4 kupoteza makaazi yao tangu Agosti mwaka jana, huku vurugu za wanamgambo zikiongezeka katika eneo la mashariki, ambako makundi ya wapiganaji yako mashughuli.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef