1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna mitihani ya kitaifa nchini Uganda kwa mwaka wa 2021

15 Novemba 2021

Bodi ya mitihani Uganda imefahamisha kuwa mwaka huu haikuandaa mitihani ya kitaifa na kwa hiyo wanafunzi waliokuwa katika madarasa husika wasubiri hadi mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/431JY
Liberia Monrovia 2013 | Studenten & Prüfung
Picha: picture-alliance/dpa/A. Jallanzo

Bodi hiyo imewataka wanafunzi waliokuwa katika madarasa ya kufanya mitihani ya kitaifa wasubiri hadi mwaka ujao.

Kulingana na bodi hiyo, idadi kubwa ya wanafunzi watahiniwa hawakuhudhuria masomo yalioendeshwa na baadhi ya shule kupitia mitandaoni.

Kwa hiyo hapatakuwa na usawa iwapo mitihani itafanyika bila wanafunzi wote kuandaliwa ipasavyo kufanya mitihani hiyo.

Hii ina maana kuwa wanafunzi ambao wangetahiniwa  watapoteza miaka miwili ya masomo yao kwani hata shule zikifunguliwa Januari mwakani, watashiriki masomo kabla ya kuandaliwa kama watahiniwa.

Kulingana na ripoti ya shirika la Umoja Mataifa linalowashughulikia watoto, Uganda ndiyo taifa ambalo limefunga shule zake kwa muda mrefu zaidi duniani kutokana na hatua za kudhibiti janga la COVID-19.