1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna kurudi EU iwapo Uingereza itajitoa

19 Juni 2016

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ameonya Jumapili (19.06.2016) hakutakuwepo na fursa nyengine ya kurudi katika Umoja wa Ulaya iwapo nchi hiyo itaamuwa kujitowa katika umoja huo wakati wa kura ya maoni.

https://p.dw.com/p/1J9Zd
Picha: picture-alliance/dpa/S. Lecocq

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ameonya Jumapili (19.06.2016) hakutakuwepo na fursa nyengine ya kurudi katika Umoja wa Ulaya iwapo nchi hiyo itaamuwa kujitowa katika umoja wakati wa kura ya maoni.

David Cameron kiongozi wa serikali ya kihafidhina nchini Uingereza ameliambia gazeti la "Sunday Times" kwamba hakutakuwepo na uwezekano kwa nchi yake kurudi tena katika Umoja wa Ulaya iwapo hapo Alhamisi wananchi wengi wataamuwa kujitowa.Amesema hakutakuwepo na fursa ya pili kuamuwa juu ya dhima ya Uingereza katika umoja huo na kwamba "huu ni uamuzi usiotengulika ambao utakuwa na taathira mbaya sana kwa uchumi wa Uingereza."

Akizungumza na gazeti jengine la Sunday Telegraph waziri mkuu huyo ameonya juu ya hatari za kukubaliana na dira ya kampeni ya kujitowa ya kiongozi wa chama cha Uhuru cha Uingereza UK Independence Nigel Farage ambaye amesema anataka kuirudisha nyuma Uingereza na kuwagawa badala ya kuwaunganisha Waingereza wakati pande zote mbili zikijiandaa kutumia nguvu zao za mwisho kabla ya kufanyika kura hiyo ya maoni hapo Alhamisi.

Kampeni imehamia katika vyombo vya habari kutokana na kusitishwa kwa mikutano mikubwa ya hadhara kufuatia kuuwawa kwa mbunge wa chama cha Labour Jo Cox hapo Alhamisi.

Cameron amemsifu dira ya huruma ya Uingereza shirikishi iliokuwa ikitetewa na mbunge huo Jo Cox ambaye aliunga mkono hadharani kampeni ya kubakia Umoia wa Ulaya tafauti na Farage na wengine wanaopigania kujitowa katika umoja huo wenye nchi wanachama 28.

Taathira ya mauaji ya mbunge

Haiko wazi iwapo kutakuwepo na taathira yoyote ile ya mauaji ya kutisha ya Cox kwa kura hiyo ya maoni.Mwanaume mwenye umri wa miaka 52 amefunguliwa mashtaka ya mauaji ya mama huyo.Wakati alipoulizwa jina lake hapo Jumamosi jibu lake lilikuwa "kifo kwa wasaliti,uhuru kwa Uingereza."

Mbunge wa chama cha Labour aliyeuwawa Jo Cox.
Mbunge wa chama cha Labour aliyeuwawa Jo Cox.Picha: Reuters/Press Association

Kampeni ya kujitowa inayoongozwa na meya wa zamani wa London Boris Johnson pia imeyageukia magazeti mashuhuri ya Jumapili kushinikiza hoja zake.Johnson ameyaambia magazeti ya Sun na Sunday kwamba kujitowa kwa Uingereza kunawapa wapiga kura fursa ya mwisho kubadili maisha ya Uingereza kuwa bora zaidi.Amesema itatowa taarifa ambayo idadumu kwa miaka mingi.

Awali Johnson alikuwa amepanga kufanya mkutano mkubwa wa hadhara hapo Jumapili lakini umefutwa baada ya kuuwawa kwa Cox.Bunge limeitisha kikao maalum hapo Jumatatu ya kumbukumbu kwa heshima kwa mbunge huyo.

Tahariri za magazeti Jumapili zimetowa uzito kwa suala hilo ambapo Sunday Times na Sunday Teleghraph zimewahimiza wapiga kura kujitowa Umoja wa Ulaya wakati Observer na Mail yameidinisha kubakia katika umoja huo.

Pande zote zinatazamiwa kuanza tena kmapeni muda mfupi kabla ya kura hiyo ya maoni hapo Alhamisi.Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba pande zote mbili hazotutumia maneno makali katika siku hizo za mwisho kwa sababu ya huzuni iliyoletwa na kifo cha Cox.

Kosa la kihistoria

Waziri wa mambo ya Kigeni wa Luxembourg Jean Asselborn amesema kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya kunaweza kusababisha kuchukuliwa hatua kama hiyo na mataifa mengine wanachama katika eneo la Ulaya Mashariki.

Waziri wa mambo ya nje wa Luxemburg Jean Asselborn.
Waziri wa mambo ya nje wa Luxemburg Jean Asselborn.Picha: picture-alliance/dpa/J. Warnand

Asselborn amenukuliwa akisema hayo alipozungumza na toleo la gazeti la Jumapili la hapa Ujerumani "Tagesspiegel am Sonntag". Amesema lilikuwa kosa la kihistoria kwa Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron hata kufikiria juu ya kuitisha kura hiyo ya maoni, kuhusu uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya.

Aidha ameongeza kuwa hata kama Uingereza itaamua kuendelea kusalia katika Umoja wa Ulaya katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Juni 23, hakutaondosha tatizo lililosababisha mtazamo hasi wa Waingereza dhidi ya Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP/AP

Mhariri : Sudi Mnette