Mazungumzo kuendelea leo jioni.
12 Agosti 2008Wakati mazungumzo juu ya kutatua mgororo wa kisiasa nchini Zimbabwe yanatarajiwa kuendelea leo jioni, shirika la kutetea haki za binadamu duniani, Human Rights Watch limetoa mwito kwa viongozi wa kusini mwa Afrika juu ya kuishinikiza serikali ya Mugabe ili ikomeshe umwagaji damu unaondelea nchini Zimbabwe.
Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch limetoa mwito huo leo katika ripoti yake juu ya kuandamwa wapinzani na wanaharakati wa kisiasa nchini Zimbabwe.
Wakati mazungumzo juu ya kugawana mamlaka yanatarajiwa kuendelea jioni ya leo baina ya wawakilishi wa serikali ya Mugabe na wa chama cha upinzani MDC, shirika hilo la kutetea haki za binadamu lenye makao mjini New York limekilaumu chama kinachotawala nchini Zimbabwe Zanu PF na wafuasi wake kwa kuendeleza mauji, kuwashumbulia na kuwatia ndani wabunge wa chama cha upinzani na wanaharakati wengine wa kisiasa.
Kutokana na madai hayo asasi hiyo ya kutetea haki za binadamu inawataka viongozi wa nchi za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC wawe na msimamo thabiti kwenye mkutano wao wa jumamosi ijayo katika kupinga kukiukwa haki za binadamu nchini Zimbabwe.
Shirika la Human Rights Watch limesema jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC inapaswa kuhakikisha kwamba polisi ya Zimbabwe inavunja haraka, kambi na vituo vya mateso vyote vilivyopo nchini kote.
Wakati huo huo msuluhishi katika mgororo wa Zimbabwe rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini anaetarajiwa kuchukua uenyekiti wa jumuiya ya SADC kwenye mkutano wa jumamosi amekuwa anajaribu kuwashawishi rais Robert Mugabe na viongozi wa upinzani wafikie makubaliano juu ya mapendekezo ya kugawana mamlaka ili kuutatua mgogoro wa nchi yao.
Mazungumzo juu ya mgororo huo yanatarajiwa kuendelea leo jioni.Lakini wawakilishi wa chama cha Mugabe Zanu PF na wa chama cha upinzani MDC bado wanatofautiana juu ya ugawanaji wa mamlaka katika serikali mpya. Mafanikio ya mazungumzo hayo yatatoa mchango mkubwa katika kuweka mazingira ya kuujenga upya uchumi wa Zimbabwe.
Lakini mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la HRW, kanda ya Afrika Georgette Gagnon amedai kuwa chama cha Zanu PF kinaendelea na matendo ya umwagaji damu na hivyo kinahujumu uadilifu wake.
Mkurúgenzi huyo amemtaka rais Mbeki aweke mkazo katika kuleta suluhisho la kudumu badala ya kutafuta suluhisho la muda tu. Lakini rais Mbeki amesema kuchukua msimamo mkali dhidi ya rais Mugabe kutafanya mvutano uwe mkubwa zaidi na kuweza kuathiri juhudi za kuleta suluhisho.