Haiti: Zoezi la kuwatafuta manusura lakamilika
23 Januari 2010Matangazo
Serikali ya Haiti imekamilisha zoezi la kuwatafuta na kuwaokoa watu
waliokwama katika vifusi kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea
nchini humo wiki iliyopita.
Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uratibu wa Misaada ya Kibinaadamu, imeeleza kuwa hadi sasa watu 132 wameokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi.
Jana Ijumaa watu wawili waliokolewa wakiwa hai katika mji mkuu wa nchi hiyo, Port-au-Prince, siku 10 baada ya tetemeko hilo kutokea. Watu hao, mwanamke mwenye umri wa miaka 84 na kijana mwenye umri wa miaka 22 walikuwa wadhaifu sana, lakini sasa wanaendelea vizuri.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na Jeshi la Marekani ambao ni watoaji wakubwa wa misaada nchini Haiti zimetiliana saini mpango wa kuendelea kutolewa misaada ya dharura. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kiasi watu 100,000 wameuawa katika tetemeko hilo
la ardhi na 200,000 wamejeruhiwa na wengine milioni moja wamepoteza makaazi yao.