HAITI: Wafuasi na wapinzani wa Rais kuvamiana
19 Januari 2004Matangazo
Mtu mmoja ameuliwa na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa katika mapambano baina ya wafuasi na wapinzani wa Rais Jean-Bertrand ARISTIDE wa Haiti katika mji mkuu Port-au-Prince. Polisi wanadai kuwa mfarakano huo ulianza kwa kurushiana risasi baada ya wafuasi wa ARISTIDE kujaribu kuzuwia wapinzani wapatao elfu 4 waliokusanyika kupinga utawala wa kiongozi huyo. Mashambuliano hayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa na wakati huo huo maandamano zaidi ya kumtaka padiri huyo wa zamani kujiengua madarakani yakifanyika. Wapinzani wanamtuhumu Rais Jean Bertrand ARISITDE kwa matumizi mabaya ya madaraka na kushindwa kutimiza ahadi zake za kuondoa umaskini nchini humo. Analalamikiwa pia kwa kuchelewesha uchaguzi uliokuwa ufanyike mwaka jana na athari zake zikidaiwa kusababisha mpaka sasa vifo vya watu wasiopungua 46.