1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

kuna njama dhidi ya demokrasia Iraq

11 Juni 2018

Imam maarufu katika siasa za  Iraq Moqtada al-Sadr amewataka Wairaq kuungana badala ya kuchoma masanduku ya karatasi za kura na kutaka kurejelewa kwa uchaguzi wa Mei 12 ulioshindwa na upande wake.

https://p.dw.com/p/2zHBe
Münchner Sicherheitskonferenz Haider al-Abadi
Picha: picture alliance/dpa/A. Gebert

Usemi wa al-Sadr unakuja baada ya jumba moja kulikohifadhiwa nusu ya karatasi za kura za Baghdad katika uchaguzi wa bunge wa Iraq kuteketea Jumapili, siku chache tu baada ya bunge kutaka kura za nchi nzima zihesabiwe upya.

"Wacheni kupigania viti, nyadhifa, umaarufu, mamlaka na uongozi," aliandika mhubiri huyo katika taarifa iliyotolewa na afisi yake.

Uhalali wa uchaguzi huo ulikuwa tayari unatiliwa shaka kwani chini ya asilimia 45 ya wapiga kura walijitokeza kushiriki zoezi hilo, hiyo ikiwa ni idadi ndogo zaidi ya wapiga kura kuwahi kurekodiwa na madai ya wizi wa kura yakaanza kuibuka mara tu baada ya kura.

Waziri Mkuu Haider al-Abadi ameuelezea moto huo kama njama dhidi ya demokrasia ya Iraq.

Msemaji asema moto ulikuwa kwenye bohari moja tu

"Kuchoma mabohari ya kura, ni njama ya kulidhuru taifa na demokrasia yake. Tutachukua hatua zote zinazohitajhika na kuwaadhibu vikali wale wote wanaoendea kinyume usalama wa taifa na raia wake," alisema Waziri Mkuu Haider al-Abadi katika taarifa yake.

Waziri Mkuu huyo ameongeza kwamba wataalam watafanya uchunguzi na watoe ripoti kuhusu chanzo cha moto huo.

Irak, Bagdad: Depot mit ausgefüllten Stimmzetteln in Flammen aufgegangen
Mabohari yaliyokuwa yanahifadhi masanduku ya kura yaliteketeaPicha: Reuters/K. Al-Mousily

Msemaji wa Wizara ya Usalama wa ndani alisema moto huo ulikuwa kwenye bohari moja tu kati ya mabohari 4 katika eneo hilo. Kituo cha televisheni cha taifa kilisema masanduku yaliyokuwa na karatasi za kura yaliondolewa na kupelekwa sehemu nyengine chini ya ulinzi mkali. Baadae Waziri wa Usalama wa ndani Qasim al-Araji alikiambia kituo kimoja cha televisheni nchini humo kwamba "hata sanduku moja halikuchomeka."

Spika wa bunge la Iraq Salim al-Jabouri alisema moto huo katika mabohari hayo ulianzishwa kusudi ili kuficha wizi wa kura. "Uhalifu wa kuteketeza mabohari yaliyo na karatasi za kura ni jambo la kusudi na uhalifu uliopangwa unaolenga kuficha wizi, kudanganywa kwa Wairaq na kubadilisha nia na chaguio lao," alisema Jabouri.

Spika huyo alitaka kuandaliwa upya kwa kura hiyo baada ya kuthibitishwa kwamba kulikuwa na wizi wa kura, matokeo yalibadilishwa na kulikuwa na njama ya wazi ya kuibadili nia na chaguo la Wairaq. Hatua hiyo ya kutaka kura hiyo iandaliwe upya iliungwa mkono na Makamu wa Rais Iyad Allawi.

Ndiyo mara ya kwanza Wairaq kupiga kura kwa njia ya kielektroniki

Waziri Mkuu al-Abadi, ambaye muungano wake ulichukua nafasi ya tatu katika uchaguzi huo, alisema uchunguzi huru wa serikali ulibaini makosa makubwa na ukailaumu tume huru ya uchaguzi ya Iraq kwa makosa hayo.

Irak Najaf Wahlurnen
Baadhi ya viongozi walikuwa wanataka kura zihesabiwe upya IraqPicha: Reuters/A. al-Marjani

Tume hiyo ya uchaguzi ilikuwa imetumia vifaa vya kielektroniki kujumuisha matokeo ila bunge lilitoa amri ya kuhesabiwa kwa kura zote kwa mkono. Huko kuhesabiwa upya kwa kura ni kinyume cha yale anayotaka muhubiri Moqtada al-Sadr, ambaye ni adui wa tangu jadi wa Marekani na ambaye upande wake ulishinda idadi kubwa ya viti katika uchaguzi huo. Mmoja wa wasaidizi wake wakuu alisema kwamba baadhi ya watu wanajaribu kuuendea kinyume ushindi wa muhubiri huyo.

Msemaji wa Baraza Kuu la Mahakama Abdel-Sattar Bairaqdar, alisema kwamba baraza hilo limewateua majaji watakaochukua jukumu la tume huru ya uchaguzi lililouendesha uchaguzi wa Mei 12 ulioshuhudia mfumo wa kielektroniki wa upigaji kura kutumika kwa mara ya kwanza nchini Iraq. Kulingana na vyombo vya habari, majaji tisa ndio watakaohusika katika kuhesabu upya kura hizo.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman