Hafla maalum ya kijeshi kumuaga Angela Merkel
2 Desemba 2021Baada ya kuwa kansela wa Ujerumani kwa miaka 16, hatimaye kansela Angela Merkel anasema kwaheri. Lakini bado atasalia ofisini kama kiongozi wa mpito hadi kansela mpya atakapoidhinishwa .
Soma: Vyama vya Ujerumani vyafikia makubaliano ya kuunda serikali mpya
Kwenye hafla ya leo, Merkel atakuwa mgeni rasmi wa dhifa hiyo maalum ya kijeshi ambayo imeandaliwa mahsusi kwa niaba yake.
Soma: Merkel aacha urithi wa mchanganyiko Afrika
Hafla hiyo kwa jina "Großer Zapfenstreich" au Big tattoo kwa Kiingereza ndiyo hafla ya hadhi ya juu zaidi ya kijeshi nchini Ujerumani. Hujumuisha gwaride la wanajeshi, maonesho maalum, muziki kutoka kwa wanajeshi Pamoja na mahanjam ya kila aina ya kijeshi kwa upekee na usahihi wake.
Hafla ya kijeshi kuwaaga makansela, marais na mawaziri wa kijeshi ina historia ndefu nchini tangu karne ya 16. Enzi hizo hafla hiyo iliyoandaliwa katika kambi za kijeshi ziliandamana na unywaji pombe na mchezo wa kamari.
Hata hivyo baadhi wanahisi ni hafla isiyofaa kwani wanaihusisha na enzi za nyuma zilizojaa kiza.
Ujerumani: Scholz akubaliana na Kijani, FDP kuanza mazungumzo ya kuunda serikali
Lakini kando na hafla hiyo ni kwamba miongoni mwa miziki ambayo Merkel amechagua kuchezwa kwenye hafla hiyo imewashangaza wengi.
Sawa na watangulizi wake, Merkel pia ameruhusiwa kuchagua nyimbo tatu ambazo wanajeshi watacheza wakati wa gwaride.
Mbili kati ya muziki ambazo Merkel alichagua zimewashangaza wengi. Moja ukiwa ni "Mungu Mtakatifu, tunalisifu jina lako”. Chaguo hili linakisiwa ni kutokana na mizizi ya Kikristo ya chama chake Pamoja na ulezi au ukuaji wake chini ya kasisi mprostenti kama baba.
Chaguo lake la pili ni "Fur mich, soll's rote Rosen regnen". Nikitafsiri moja kwa moja ni sawa na kusema "Yapasa ninyeshewe waridi nyekundu”. Wimbo ambao ulikuwa kama matamanio ya kijana ukiwa na maneno kama vile nipate vyote ama nikose vyote.
Chaguo lake jingine ni kibao kilichotia fora mwaka 1974 Ujerumani ya Mashariki chake Nina Hagen "Du hast den Farbfilm vergessen” yaani umesahau filamu ya rangi.
Japo serikali haikuupiga marufuku muziki huo, ulieleweka na wengi kama ukosoaji wa enzi za giza na dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Ujerumani ambayo filamu ilikuwa jambo la nadra.
Angela Merkel mwenye umri wa miaka 67 atastaafu kwenye siasa atakapoondoka rasmi ofisini. Lakini ikiwa chaguo la muziki na mishororo au mistari yake ni ya kuashiria chochote, basi huenda huo si mwisho wa safari yake kisiasa.
(DW)
Mwandishi: Silke Wünsch
Tafsiri: John Juma
Mhariri: Chilumba Rashid