1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haaland asema ni fahari kubwa kujiunga na Man City

13 Juni 2022

Vilabu viwili vikubwa vya England leo vimetanua misuli kwa kutangaza kuwasajili mastaa wawili wakubwa. Erling Haaland ametua Manchester City wakati Darwin Nunez ametangazwa kuwa atajiunga na Liverpool

https://p.dw.com/p/4Cdi2
Bildkombo | Pep Guardiola und Erling Haaland
Picha: Oli Scarff/Ina Fassbender/AFP/Getty Images

Manchester City imemtambulisha rasmi mshambuliaji wa Norway Erling Haaland wakati Liverpool imeipata saini ya mshambuliaji wa Benfica Darwin Nunez. Haalanda amesema uhamisho wake kutoka Borussia Dortmund kwenda Man City ni hatua nzuri kabisa kwa taaluma yake. Halaand amesaini mktaba wa miaka mitano na kufuata nyayo za baba yake Alfie Inge Haaland, aliyeichezea City kati ya 2000 na 2003.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye alisajiliwa kwa pauni milioni 51 amesema ni siku ya fahari kwake na familia yake. Mara zote amekuwa akiitazama City na hasa katika misimu ya karibuni. Amesema anataka kufunga mabao, kushinda mataji, na kuimarika kama mchezaji kandanda. Na anapenda filisofia ya Pep Guardiola "ndiyo. bila shaka, kama sio hivyo, nisingekuja hapa. kwa hiyo ndiyo. napenda mtindo wao. Napenda kandanda la kushambulia, napenda aina ya msisimko tulionao wakati City inapocheza kandanda. Hicho ndicho ninachokipenda sana kwa hiyo nadhani nitakuwa vizuri hapa."

Nao Liverpool wamefikia makubaliano na Benfica ya kumsajili mshambuliaji wa Uruguay Nunez mwenye umri wa miaka 22 kwa kiasi cha awali cha euro milioni 75 ambazo zitaongezeka hadi milioni 100 kwa kutegemea na mambo mengine. Liverpool imevunja benki kumpata mchezaji huyo, ambapo rekodi ya awali iliwekwa ya kumpata beki wa kati Mholanzi Virgil van Dijk mwaka wa 2018. Inatarajiwa kuwa atasaini mkataba wa miaka sita na Liverpool.

afp, ap