Guterres:Zaidi ya watu milioni 780 wanateseka kwa njaa
24 Julai 2023Mkutano huo wa mifumo ya chakula unajiri wakati kukiwa na uhaba unaoongezeka wa chakula kote ulimwenguni, huku mashirika ya Umoja wa Mataifa yakionya kuhusu ongezeko la idadi ya watu wanaoteseka kwa kiwango kikubwa cha njaa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika ufunguzi wa mkutano huo kuwa katika ulimwengu wenye chakula cha kutosha, inakasirisha kuwa watu wanaendelea kuteseka na kufa kwa njaa.
Amesema zaidi ya watu milioni 780 wanateseka kwa njaa kote ulimwenguni, hata wakati ambapo karibu theluthi moja ya chakula ulimwenguni kinaharibiwa au kupotea.
Soma pia:UN yahofia mzozo wa chakula Sahel
Amesema watu milioni 462 wana uzito hafifu na bilioni mbili ni wanene kupindukia.
Mkutano huo unayaleta pamoja wawakilishi watatu kutoka mashirika ya chakula ya Umoja wa Mataifa yenye makao yao makuu mjini Rome, Shirika la Chakula na Kilimo - FAO, Shirika la Mfuko wa Kimataifa wa Kilimo na Maendeleo- IFAD na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP, pamoja na wakuu wa nchi, wawakilishi wa serikali na wajumbe.