Guterres ataka usitishaji haraka mapigano Syria
26 Februari 2018Wakati huo huo raia walionaswa katika mapigano makali nchini Syria bado wanasubiri misaada ya chakula na madawa leo Jumatatu baada ya majeshi ya serikali kushambulia eneo la Ghouta mashariki licha ya azimio la Umoja wa mataifa kutaka kusitishwa mapigano.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesifu baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuidhinisha azimio hilo Jumamosi iliyopita baada ya siku kadhaa za mjadala uliochukua muda mrefu, lakini amesisitiza kwamba azimio la Baraza hilo la Usalama litakuwa tu na maana iwapo litatekelezwa kwa dhati, na ndio sababu amesema anatarajia azimio hilo litatekelezwa na kuendelezwa.
Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametoa wito akitaka kutekelezwa mara moja makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Syria. Mogherini amesema kabla ya kikao cha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwamba azimio la Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu na inayotia moyo, lakini ni hatua ya kwanza.
Watu zaidi ya 500 wauwawa
Zaidi ya watu 500 wameuwawa katika mashambulizi makubwa ya majeshi ya rais Bashar al-Assad mbayo yameshambulia eneo hilo la Ghouta lililoko ukingoni mwa mji mkuu Damascus kwa wiki sasa.
Baada ya siku kadhaa za mivutano ya kidiplomasia, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumamosi liliidhinisha azimio linalotaka kusitishwa mapigano kwa muda wa siku 30 nchini Syria, bila kuchelewa, kuruhusu upelekaji wa misaada na kuwaondoa wagonjwa na waliojeruhiwa. Mkaazi mmoja wa mji wa Damascus hata hivyo ameonesha shaka kuhusiana na makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
"Usitishaji huu wa mapigano ni sawa na mwingine uliopita na tutaona utavunjwa na kukiukwa. Hiki ni kichekesho ambacho hatupaswi kukiamini, na hii ni ya zamani, iwapo inarudiwa sisi ndio tunashambuliwa. Huoni watoto, watu wazima, wanawake na wanafunzi? Nani tunapaswa kumsikitikia, kwa wapinzani?, Balozi wa Syria katika Umoja wa mataifa al-Ja'afar, Mungu amlinde , alisema kuna watu milioni nane ambao hatuwajali, lakini tunajali tumbuli 700."
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria, limesema kiasi ya raia 14 ikiwa ni pamoja na watoto wameuwawa katika mashambulizi ya anga jana Jumapili, na kufikisha jumla ya watu waliouwawa kuwa 530, miongoni mwao zaidi ya watoto 130.
Mfanyakazi wa shirika la kutoa misaada mjini Douma, alinukuliwa na shirika la misaada la Uingereza la Save the Children, akisema kusita kwa muda kwa mashambulizi ya mabomu kumesaidia watu kujitokeza baada kujificha kwa muda wa wiki nzima.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Josephat Charo