Guterres asema mashambulizi yanapaswa kusita Syria
26 Februari 2018Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka utekelezaji mara moja wa azimio linalotaka kusitishwa mapigano kwa muda wa siku 30 nchini Syria, wakati shambulio jingine linaloshukiwa kuwa la silaha za sumu limesabisha mtoto mmoja kufariki katika eneo hilo.
"Ghouta mashariki haiwezi kusubiri. Muda umefika sasa kusitisha mauaji haya ya jahanamu hapa duniani," Antonio Guterres alikiambia kikao cha ufunguzi cha 37 cha baraza la haki za binadamu la Umoja wa mataifa mjini Geneva.
Azimio la baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa siku ya Jumamosi limeleta matumaini kwamba mashambulizi ya wiki nzima yaliyofanywa na jeshi la serikali linaloungwa mkono na Urusi ambayo yamewauwa raia zaidi ya 500 huenda yakafikia mwisho.
Lakini wakati mashambulizi makali yalipungua kidogo mwishoni mwa juma, ndege za kijeshi zimeendelea na mashambulizi yao na makombora bado yanarushwa Ghouta mashariki. Miongoni mwa wahanga wa hivi karibuni ni watu tisa wa familia moja waliouwawa pale nyumba yao mjini Douma, mji mkuu wa eneo hilo, ilipoporomoka na kuwaangukia.
"Raia tisa kutoka familia moja wameuwawa katika mashambulizi ya majeshi ya serikali mjini Douma, usiku wa manane," Rami Abdel Rahman, mkuu wa shirika la kuangalia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Baraza la taifa la usalama
Rais wa Urusi Vladimir Putin wakati huo huo amejadili hali katika eneo la mashariki mwa Ghouta nchini Syria na baraza la usalama la taifa, shirika la habari la TASS limesema leo, likimnukuu msemaji wa serikali Dmitry Peskov. Peskov amesema kwamba baraza la usalama la Urusi limeeleza wasiwasi wake juu ya vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na waasi wa Syria, kwa mujibu wa shirika la habari la TASS.
Jana Jumapili, mtoto mmoja alifariki na wengine 13 walipata matatizo ya kupumua na kuonesha ishara za mara kwa mara za shambulio la gesi ya Klorini baada ya shambulio la majeshi ya serikali katika mji wa Al-Shifuniyah, limesema shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria. Urusi ilikanusha ripoti hizo za mashambulizi ya silaha za sumu kuwa ni hadithi zisizo na maana. Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alisema:
"Baadhi ya maandiko ya kupakana matope tayari yameonekana katika vyombo vya habari yakisema sumu ya klorini ilitumika kama silaha jana ama asubuhi ya leo huko mashariki mwa Ghouta. Ilifanyika akinukuliwa mtu mmoja ambaye hakutajwa jina anayeishi Marekani. Nataka kuwakumbusha kwamba jana maafisa wa Urusi walishaonya juu ya uchokozi na bila shaka tayari tunaona katika majimbo ya kusini mwa jamhuri ya Kiarabu ya ,Syria ambako Marekani , nina hakika, inajaribu kuweka hali ya Taifa tofauti na kuigawa Jamhuri wa Kiarabu ya Syria."
Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amemweleza rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan leo kuwa pendekezo la Umoja wa mataifa la kusitisha mapigano nchini Syria linapaswa kuhusisha nchi nzima, ikiwa ni pamoja na jimbo la Afrin ambako Uturuki inafanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kikurdi.
Katika mazungumzo kwa njia ya simu baina ya viongozi hao wawili, Macron alisema usitisjaji mapigano wa siku 30, unahusisha ardhi yote ya Syria, ikiwa ni pamoja na Afrin, na ni lazima yatekelezwe kila mahali na kila mmoja bila kuchelewa, imesema ofisi ya rais.
Mwandishi Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Josephat Charo