1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guterres aona 'upepo wa matumani' Afrika

9 Februari 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema chaguzi nyingi za amani na mapatano barani Afrika ni ishara za "upepo wa matumaini" barani humo, na kwamba Afrika inageuka mfano wa kutatua na kuzuwia migogoro.

https://p.dw.com/p/3D3Pc
UN-Klimakonferenz 2018 in Katowice, Polen | Antonio Guterres, UN-Generalsekretär
Picha: Getty Images/AFP/J. Skarzynski

Guterres alikuwa akizungumza pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika (AU) katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, ambako wakuu wa mataifa 55 wanachama watakutana Jumapili.

"Huu ndiyo wakati ambamo upepo wa matumaini unavuma kote Afrika. Tumeshuhudia maridhiano kati ya Ethiopia na Eritrea, tumeona makubaliano ya amani....nchini Sudan Kusini na CAR (Jamhuri ya Afrika ya Kati)," alisema Guterres.

"Tunashirikiana kuona iwapo tunaweza kuelekea upande sawa nchini Libya. Tumeshuhudia uchaguzi nchini Madagascar, DRC na Mali ambapo watu walikuwa wanatabiri utasababisha majanga na vurugu na mwishowe ulifanyika katika muktadha wa amani," aliongeza.

Äthiopien AU-Gipfel in Addis Adeba
Viongozi wakuu wa Afrika wanakutana Addis Ababa Jumapili katika mkutano wa kilele utaozingatia hali ya wakimbizi barani Afrika.Picha: Getty Images/AFP/M. Tewelde

Ethiopia na Eritrea mwaka uliopita zilihitmisha vita baridi vilivyodumu kwa miongo miwili, huku Sudan Kusini ikijaribu kutekeleza makubaliano ya karibuni zaidi katika orodha ndefu ya makubaliano ya amani ya kukomesha mgogoro wa umuagaji damu uliodumu kwa miaka mitano.

Jamhuri ya Afrika ya Kati wiki hii ilifikia makubaliano ya mani kati ya serikali na makundi 14 ya wanamgambo, na kuimarisha matumaini ya kukomesha mgogoro ulioikumba nchi hiyo tangu 2012, na kuzusha mzozo uliosababisha vifo vya maelf ya watu na zaidi ya milioni kupoteza makazi yao.

"Mazingira yote haya yalitimizwa kupitia mchanganyiko wa juhudi za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ... kuhakikisha silaha zitanyamza kuanzia 2020 na kuendelea kwenye bara la Afrika," alisema Guterres.

"Ninaamini Afrika inageuka kuwa mfano ambako inawezekana kutatua migogoro na kuzuwia migogoro na natumaini upepo huu wa matumaini unaweza kusogea katika maeneo mengine ya dunia."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Zainab Aziz