Guantanamo Bay. Waislamu wakasirishwa na kiburi cha kuidharau Koran kulikofanywa na wanajeshi wa Marekani huko Guantanamo Bay.
14 Mei 2005Ripoti kwamba wachunguzi wa Kimarekani katika jela ya Guantanamo Bay, nchini Cuba wameharibu kitabu cha Koraan Tukufu, zimesababisha maandamano makubwa katika maeneo ya nchi za Asia na duniani kote waliko Waislamu. Kiasi cha watu 16 wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika siku ya nne ya maandamano dhidi ya Marekani nchini Afghanistan.
Waislamu wamekasirishwa na ripoti kuwa wachunguzi wa Marekani walikiweka kitabu hicho kitakatifu chooni na hata kutupa kabisa chooni kimoja kati ya vitabu hivyo.
Viongozi wa kidini nchini Afghanistan waliwaambia waumini kuwa maandamano hayo ni halali, lakini waepuke ghasia.
Maandamano yameripotiwa kufanyika huko Pakistan , Indonesia , pamoja na maeneo ya Wapalestina.
Akizungumzia maandamano hayo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleeza Rice ametoa wito wa utulivu. Bibi Rice amesema utafanyika uchunguzi kuhusiana na madai hayo. Iwapo itagundulika kuwa kweli, wale waliohusika wataadhibiwa.