1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Guaido awataka Wavenezuela kuandamana

2 Februari 2019

 Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela aliyejitangaza rais wa mpito, Juan Guaido amewataka wananchi wa Venezuela na duniani kote kuandamana, wakati ambapo mzozo wa kisiasa unaendelea nchini humo.

https://p.dw.com/p/3Cc8T
Venezuela Oppositionsführer Juan Guaido
Picha: Reuters/C. Garcia Rawlins

Guaido ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba wanaandamana, huku wakiungwa mkono na jumuia ya kimataifa. Maandamano hayo yameitishwa kwa lengo la kumtaka Rais Nicolas Maduro aondoke madarakani na aitishe uchaguzi mpya. Wafuasi wa Maduro pia wanatarajiwa kuandamana leo Jumamosi.

Maandamano hayo yanatarajiwa pia kufanyika Marekani, Uhispania, Peru, Mexico na Argentina, ambako Wavenezuela wengi wanaishi. Nchini Uhispania ambako kuna kiasi ya Wavenezuela 400,000, maandamano yanafanyika katika miji kadhaa.

Marekani yamtambua Guaido

Marekani ilitangaza kumtambua Guaido, mwenye umri wa miaka 35 kama kiongozi halali wa Venezuela, kama ambavyo zimefanya nchi kadhaa za Magharibi na Jumuia ya Mataifa ya Amerika, OAS, yenye jumla ya nchi 35. Jumamosi iliyopita, mataifa kadhaa ya Ulaya yalisema yatamtambua Guaido kama rais wa mpito, iwapo hakutakuwa na mipango ya kufanyika uchaguzi mpya ndani ya siku nane.

Wakati huo huo, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la anga la Venezuela ameiasi serikali ya Rais Maduro na ametangaza kuwa anamtambua Guaido kama rais wa mpito. Jenerali Francisco Yanez, mjumbe wa kamandi ya kikosi cha anga amewataka maafisa wengine wa kijeshi wamuunge mkono Guaido.

Venezuela Krise | mutmaßliches Twitter-Video von Francisco Yanez, Luftwaffe
Jenerali Francisco YanezPicha: twiter.com

Akizungumza katika video iliyochapishwa katika mtandao wa Twitter na YouTube, jenerali huyo amesema kipindi cha mpito kuelekea kwenye demokrasia kimekaribia. Hata hivyo, kamandi hiyo imemshutumu Jenerali Yanez kwa uhaini. Yanez ni jenerali wa kwanza wa Venezuela kumtambua Guaido, tangu alipojitangaza kuwa rais wa mpito, Januari 23.

Yanez amekataa kusema kama bado yuko Venezuela au ameondoka nchini humo, ingawa amedai kuwa asilimia 90 ya vikosi vya usalama vinampinga Maduro.

ICRC yaonya kuhusu misaada

Hayo yanajiri wakati ambapo Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu duniani, ICRC imezungumza na Marekani kuhusu hatari za kupeleka msaada wa kibinaadamu nchini Venezuela, bila ya kuidhinishwa na vikosi vya usalama vinavyomtii Rais Maduro.

Guaido alisema ataipinga marufuku ya Maduro kuzuia msaada kwa kuziomba nchi jirani kusaidia kupeleka msafara mkubwa wenye dawa na chakula. Alexandra Bovin, anayeongoza ujumbe wa ICRC nchini Marekani na Canada amesema kamati yake imewaambia maafisa wa Marekani mipango yoyote inayopaswa kuwasaidia watu wa Venezuela, inatakiwa kulindwa kwa mazungumzo ya kisiasa.

Aidha, mkurugenzi wa ICRC anayehusika na shughuli za kimataifa, Dominik Stillhart amesema kamati hiyo itashiriki tu katika juhudi za kuratibu, ikiwa zinafanyika kwa kuzingatia makubaliano ya kimamlaka, na watashirikiana na yeyote yule mwenye mamlaka.

Symbolbild Internationales Rotes Kreuz
Nembo ya Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu duniani, ICRCPicha: picture-alliance/AP Photo/D. Vojinovic

Serikali ya Rais wa Marekani, Donald Trump ilitangaza kwamba iko tayari kupeleka misaada nchini Venezuela wakati wowote Guaido atakapoamua kuhusu hilo. Jana, mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani John Bolton aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Marekani inaendelea na mipango ya kupeleka msaada wa kibinaadamu Venezuela.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Iran, Hassan Rouhani leo ameikosoa Marekani kwa kutaka kuwa ''mtawala wa dunia'' na ameilanii vikali hatua ya Marekani kujaribu kumuondoa Maduro mshirika wa karibu wa Iran. Akizungumza na mjumbe mpya wa Venezuela nchini Iran, Rouhani amesema Wamarekani kimsingi wanayapinga mapinduzi yote maarufu na nchi zinazojitegemea na inajaribu kuzitawala kwa kuzikandamiza. Iran, Urusi, China na Uturuki zinamuunga mkono Maduro.

Ama kwa upande mwingine, Guaido ameiahidi China kwamba ataheshimu makubaliano kati ya nchi hizo mbili na kwamba yuko tayari kuanza mazungumzo na China haraka iwezekanavyo. Matamshi hayo yamechapishwa leo Jumamosi katika gezeti moja la China.

Septemba mwaka uliopita, Maduro aliizuru China ambako alisaini mikataba ya nishati na madini ya dhahabu wakati alipotafuta msaada wa China kwa ajili ya taifa lake lililokumbwa na mzozo. Guaido amesema msaada wa China ni muhimu sana katika kuimarisha uchumi wa Venezuela na maendeleo ya baadae ya nchi hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, AP, Reuters
Mhariri: Bruce Amani