Guaido ataka mahusiano na jeshi la Marekani
12 Mei 2019Guado amesema amemuagiza Carlos Vecchio, ambaye Marekani inamtambua kama balozi wa Venezuela, kuanzisha "mawasiliano ya moja kwa moja" kuelekea uwezekano wa "ushirikiano" wa kijeshi. Kauli hizo, alizotoa mwishoni mwa maandamano ya jana, ndilo ombi kubwa zaidi kuwahi kutolewa kwa Marekani kuingilia kati mzozo wa nchi hiyo unaongezeka kwa kasi.
Hapo jana, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladmir Pradino alilaani kile alichokiita kuwa ni uvamizi wa haramu uliofanywa na meli ya Marekani ya Walinzi wa Pwani katika mipaka ya Venezuela. Hakutoa ushahidi wa kuunga mkono madai hayo lakini akasema wanajeshi wa majini wa Venezuela waliilazimu kuondoka.
Katika maandamano ya jana, Guaido aliwataka wafuasi wake kutokuwa na uwoga na kuyaendeleza maandamano ya kitaifa dhidi ya Maduro, ambaye amekuwa akimuongezea mbinyo mbunge huyo tangu jaribio la mapinduzi ya kijeshi.
Karibu awatu 2,000 walifurika katika uwanja wa eneo lenye wafuasi wengi wa upinzani la mashariki mwa mji mkuu Caracas kumsikiliza Guaido, lakini hiyo ilikuwa idadi ndogo sana ikilinganishwa na maelfu ya watu walioshiriki katika maandamano ya awali.
Guaido mwenye umri wa miaka 35, ambaye anasema Maduro aliiba uchaguzi wa mwaka jana, ameongoza maandamano ya mara kwa mara na kulitaka jeshi kumtomtii Maduro, ambaye anaendelea kupata uungaji mkono kutoka kwa Urusi na China.
Wabunge 10 wa upinzani walishitakiwa kwa kujaribu kuipindua serikali mnamo Aprili 30.
Marekani na Umoja wa Ulaya wamelaani vitendo vya serikali ya Maduro dhidi ya wabunge wa upinzani.