1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juan Guaido asema hatua za Maduro hazimtishi

1 Februari 2019

Kiongozi wa upinzani Venezuela Juan Guaido amesema kikosi maalum cha jeshi la polisi, kilifika nyumbani kwake na kuitisha familia yake, huku akiinyooshea kidole cha lawama serikali ya rais Nicolas Maduro.

https://p.dw.com/p/3CYn5
Venezuela Oppositionsführer Juan Guaido
Picha: Reuters/C. Garcia Rawlins

Hatua hiyo imeongeza hofu ya usalama kwa kiongozi huyo wa upinzani Juan Guaido aliye na miaka 35, aliyejitangaza kuwa rais wa mpito wiki iliyopita, katika hatua ya kijasiri ya kuupinga utawala wa Nicolas Maduro. 

Venezuela, Caracas: Nicolas Maduro hält eine Ansprache
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro Picha: Reuters/Miraflores Palace

Akizungumza katika chuo kikuu cha Caracas, Guaido alisema kikosi hicho maalumu cha jeshi la polisi  kilikwenda nyumbani kwake kumhoji  mkewe Fabiana Rosales Guaido.

Juan Guaido ameonya kuwa maafisa hao wa usalama watawajibishwa iwapo familia yake itadhurika, na kwamba kwa sasa hawatishiki.

Hata hivyo polisi imekanusha kuhusika na tukio hilo kwa kuandika katika mtandao wake wa twitter kwamba taarifa zinazotolewa na Guaido hazina ukweli wowote.

Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amesema dunia inaangalia kinachoendelea Venezuela na Marekani haitovumilia hatua zozote za kuwadhuru wale wanaopigania uhuru na demokrasia ya Venezuela.

Juan Guaido ajaribu kuwashawishi China na Urusi wamuunge mkono

Dunia imeendelea kugawika kati ya mataifa yanayomtaka Nicolas Maduro kuendelea kuwepo madarakani na wale  wanaomshinikiza ajiuzulu huku Guaido akiendelea kujaribu kuwafikia adui zake China na Urusi.

Guaido ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ametuma barua kwa nchi zote mbili ambazo ni wakopeshaji wakuu wa kigeni wa Venezuela na wanaomuunga mkono Maduro katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya wasiwasi wa taifa hilo kutolipa deni lake.

Juan Guaido, Präsident der venezolanischen Nationalversammlung
Juan Guaido aliejitangaza rais wa mpito VenezuelaPicha: picture-alliance/P. Perez

Guaido amesema litakuwa jambo jema iwapo Urusi na China zitamuunga mkono na kubadilisha mkondo wao kwa Venezuela ambaye ni mwanachama wa Jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi OPEC. Awali wabunge wa ulaya walimtambua Guaido kama kaimu rais wa Venezuela ikiwa ni hatua moja mbele ya kumng'oa madarakani kiongozi wa kisoshalisti alioudidimiza uchumi wa Venezuela. 

Mataifa manne yalioyo na nguvu barani Ulaya Uingereza Ufaransa Ujerumani na Uhispania zimesema zitamtambua Juan Guaido iwapo rais Maduro atatangaza uchaguzi mwishoni mwa juma huku Maduro mwenyewe akisema uchaguzi utakaokuwepo ni ule wa mwaka 2025.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mahriri: Josephat Charo