Grossi awasili Iran kwa mazungumzo ya nyuklia
3 Machi 2023Grossi yuko nchini humo kwa mazungumzo na maafisa wa Iran baada ya wakaguzi wa shirika hilo kufichua chembechembe za urani zilizorutubishwa kwa kiwango cha chini kidogo tu ya silaha za nyuklia.
Ripoti ya siri ya IAEA imesema chembechembe hizo zimefikia kiwango cha asilimia 83,7 na zinakaribia viwango vya asilimia 90 zinazohitajika ili kubuni silaha za nyuklia, ziligundiliwa katika kiwanda kilichopo chini ya ardhi huko Fordo, karibu kilometa 100 kusini mwa mji mkuu Tehran.
Ziara ya Grossi inajiri huku shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Vienna likiishinikiza Iran kuongeza ushirikiano katika shughuli zake za nyuklia.
Hata hivyo Iran inaendelea kukanusha kuwa na nia ya kuwa na silaha za nyuklia na kukanusha kufanya jaribio lolote la kurutubisha madini ya urani kwa zaidi ya asilimia 60.