Grace Mugabe atolewa waranti wa kukamatwa
19 Desemba 2018
Mwanasheria anayefanya kazi na shirika la kutetea haki za binadamu la AfriForum la huko Afrika Kusini, Garrie Nel amesema amethibitishiwa na polisi kuhusu kutolewa kwa waranti huo, na kuongeza kwamba ikiwa Bi Mugabe atakanyaga kwenye ardhi ya Afrika Kusini atakamatwa.
Mwanasheria huyo vile vile ametaka mchakato wa kumtia mbaroni Grace Mugabe na kumsafirisha hadi Afrika Kusini uanze sasa.
Grace Mugabe anatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi mwanamitindo Gabriella Engels kwenye hotel moja mjini Johannesburg Agosti mwaka 2017, lakini hakushitakiwa kwa sababu alikuwa na kinga ya kidiplomasia.
Mwanamitindo huyo anadai alikuwa na vijana wawili wa Bi Mugabe kwenye hotel hiyo iliyo katika kitongoji cha matajiri cha Sandton, aliposhambuliwa na Grace Mugabe kwa kipigo bila maelezo yoyote. Bi Mugabe anasema alifanya hivyo kwa kujihami, na aliruhusiwa kurejea Zimbabwe bila kufunguliwa mashitaka. Wakati huo mmewe Robert Mugabe alikuwa bado madarakani.
Uamuzi wa kumuachia Grace walaaniwa
Uamuzi wa kumuachia huru Bi Mugabe ulipingwa na shirika la AfriForum na chama cha upinzani cha Democratic Alliance, na Julai mwaka huu, Mahakama ya Juu ya Guateng nchini Afrika Kusini iliamua kwamba kwa kuikubali kinga ya kidiplomasia ya Mugabe, serikali ya nchi hiyo ilikiuka katiba.
Grace Mugabe ambaye alipachikwa jina la utani la Gucci Grace alichukiwa sana nchini Zimbabwe kutokana na maisha yake ya anasa na kiu yake ya ushawishi wa kisiasa. Watoto wake wa kiume aliowazaa na Robert Mugabe aliyeangushwa kupitia mapinduzi ya kijeshi Novemba iliyopita, wana mtindo wa maisha sawa na ule wa mama yao.
Jeshi nalo lawamani
Huku hayo yakiarifiwa, tume iliyoundwa kuchunguza vifo vya watu 6 waliopoteza maisha katika maandamano yaliyofuatia uchaguzi mkuu wa Agosti nchini Zimbabwe, ililitwisha lawama jeshi la nchi hiyo, ikisema lilitumia nguvu kupita kiasi.
Rais Emmerson Mnangagwa aliyesoma ripoti ya uchunguzi huo, amesema vitendo vya polisi na jeshi kufyatua risasi hewani kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakisababisha kitisho cha usalama vinakubalika, lakini kuwalenga moja kwa moja kwa risasi za moto waandamanaji waliokuwa wakikimbia, hakukuwa halali.
Uchunguzi huo ulichukuliwa kama kipimo cha kuangalia ikiwa serikali ya Mnangagwa ingeweza kujitenga na matendo ya vyombo vya usalama, ambavyo vina mafungamano ya muda mrefu na utawala wa mtangulizi wake, Robert Mugabe.
Mwandishi: Daniel Gakuba/ape,rtre
Mhariri: Mohammed Khelef