1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Goodluck Jonathan kuiongoza tena Nigeria

Kabogo, Grace Patricia19 Aprili 2011

Tume ya uchaguzi ya Nigeria imemtangaza rais aliyeko madarakani nchini humo, Goodluck Jonathan kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita baada ya kupata asilimia 57 ya kura.

https://p.dw.com/p/10vu3
Rais mteule wa Nigeria, Goodluck JonathanPicha: AP

Mpinzani wake mkuu, Muhammadu Buhari, kiongozi wa zamani wa kijeshi na ambaye anatokea upande wa kaskazini, amepata asilimia 31 ya kura.

Katika hotuba yake ya kukubali matokeo, rais huyo mteule ametoa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi kuzuka kwenye eneo la kaskazini lenye Waislamu wengi.

Amesema nchi hiyo lazima iepukane haraka na mapambano ya wafuasi wa kisiasa na kwamba thamani ya maisha ya Wanigeria haiwezi kufananishwa na nia za mtu za kisiasa.

Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Nigeria, limesema kuwa nyumba, makanisa na misikiti imechomwa moto katika eneo hilo la kaskazini kutokana na matokeo hayo. Watu 300 wamejeruhiwa katika ghasia hizo na wengine 15,000 hawana makaazi.

Aidha, shirika hilo limesema watu wengi wameuawa, lakini kwa sasa haliwezi kuchapisha idadi ya waliouawa. Polisi wamesema kuwa ghasia hizo ni za kisiasa, na sio za kikabila au kidini.