1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Giuseppe Conte aapishwa kuwa waziri mkuu Italia

1 Juni 2018

Guiseppe Conte ameapishwa kuwa waziri mkuu wa serikali mpya ya Italia, baada ya kumalizika kwa mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa na uliotishia kuirejesha nchi hiyo kwenye uchaguzi mpya.

https://p.dw.com/p/2yolj
Italien, Rom: Präsident Sergio Mattarella gibt Giuseppe Conte die Hand
Picha: picture-alliance/G. Borgia

Conte - profesa wa sheria na mwanagenzi katika siasa - alichaguliwa na chama cha League kinachopinga uhamiaji na Vuguvugu la Nyota Tano kisichoupendelea Umoja wa Ulaya, kuongoza serikali ya kwanza ya wafuasi wa siasa kali katika taifa kubwa la Umoja wa Ulaya. Alikubali jukumu la kuunda serikali na kuwasilisha orodha yake ya mawaziri kwa rais wa Italia Sergio Mattarella Alhamisi jioni.

Katika hafla iliofanyika kwenye kasri la rais mjini Rome, kiongozi wa chama cha League Matteo Salvini ameapishwa kuwa waziri mambo ya ndani, huku kiongozi wa vuguvugu la Nyota tano Luigi Di Maio akila kiapo chake kama waziri wa ajira. Di Maio na Salvini pia watahudumu kwa pamoja kama manaibu waziri mkuu katika muungano huo mpya.

Serikali hiyo laazima iidhinishwe kwa kura ya bungenia ambako vyama vya Nyota Tano na League vina wingi wa wabunge katika mabaraza yote, na hivyo kuwa na uhakika wa kuidhinishwa kwa serikali hiyo. Vyama hivyo viliunda muungano wao ambao hauna uzoefu wowote kufuatia uchaguzi wa Machi 4 ambamo hakuna chama chochote kilichopata wingi wa kujitosheleza bungeni.

Rom Matteo Salvini Chef Lega Nord
Kiongozi wa chama cha League Matteo Salvin, ambaye amechukuwa wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani.Picha: Reuters/T. Gentile

Makubaliano ya dakika za mwisho

Baada ya wiki kadhaa za mivutano ya kisiasa ambayo katika wakati mmoja ilionekana kupelekea uchaguzi mpya, Rais Sergio Mattarella alimteuwa Conte kuwa waziri mkuu kwa mara ya pili katika muda wa chini ya wiki mbili na pia kuidhinisha orodha ya baraza lake la mawaziri.

Conte alirejesha mamlaka aliopewa awali ya uwaziri mkuu siku ya Jumapili, baada ya Mattarella kukataa chaguo la mpinzani wa Umoja wa Ulaya Paolo Savona kuwa waziri wa uchumi, na kusababisha kuvunjika kwa makubaliano ya kuunda serikali.

Lakini katika hatua ya kushangaza, vyama hivyo vilifufua majadiliano ya kuunda muungano na hatimaye Conte akakubali uteuzi mpya wa kuwa waziri mkuu. Aliwasilisha orodha ya mawaziri iliofanyiwa marekebisho kwa rais -- ambapo Savona alihamishiwa kwenye wizara ya masuala ya Umoja wa Ulaya, ambayo ilikubaliwa mara moja na rais huyo.

Italien Regierungsbildung | Luigi Di Maio
Luigi Di Maio, kiongozi wa chama cha Vuguvu la Nyota Tano na waziri mpya wa ajira.Picha: Getty Images/AFP/T. Fabi

Umoja wa Ulaya watuma ujumbe

Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amempongeza Conte katika wadhifa wake mpya na kumhimiza kushirikiana na wenzake wa Umoja wa Ulaya katika majadiliano ya heshima na ushirikiano aliouita tiifu.

Katika barua aliomuandikia Cote, Tusk amesema uteuzi wake umekuja katika wakati muhimu kwa Italia na kanda nzima ya Umoja wa Ulaya, akibainisha kuwa umoja na mashikamano vinahitajika ili kuvuka changamoto za pamoja na kanda hiyo.

Naye msemaji wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Mina Andreeva amesema rais wa halmashauri hiyo Jean-Claude Juncker, atakutana waziri mkuu huyo mpya wakati wa mkutano wa kilele wa mataifa saba yaliostawi zaidi kiviwanda duniani G7, unaofanyika nchini Canada wiki ijayo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe,dpae

Mhariri: Mohammad Abdul-Rahman