GHAZNI:Mateka 2 wa kike wa Korea kusini waachiwa
12 Agosti 2007Mateka wawili wa kike wa Korea Kusini waliokuwa wanazuiliwa na taleban nchini Afghanistan wameachiliwa.Hayo ni kwa mujibu wa kundi la Taleban japo maafisa wa serikali bado hawajathibitisha habari hizo.Wanawake hao wawili waliachiwa kwasababu walikuwa katika hali mbaya ya afya.Tukio hilo linatokea saa chache baada ya mazungumzo ana kwa ana kukamilika kati ya Taleban na wajumbe wa Korea Kusini.
Pande zote mbili hazijathibitisha tukio hilo.Kulingana na msemaji wa kundi la Taleban Yousuf Ahmadi baraza la uongozi lao la uongozi limamua kuwaachia huru mateka hao wa kike.Mpaka sasa huenda hawajapokelewa na upande wa serikali kwasababu ya matatizo ya usafiri.
Kundi la Taleban liliwateka wahudumu wa msaada 23 wa Korea Kusini kwenye eneo la ghasia mkoani Ghazni Julai 19 walipokuwa msafarani kuelekea mji wa Kabul.Mpaka sasa mateka wawili wa kiume wameuawa na wapiganaji hao kutisha kuwaua wengine zaidi endapo madai yao hayatatimizwa.
Wawakilishi wa kundi la Taleban na Korea Kusini walikutana Ghazni hapo jana kwa awamu ya pili ya mazungumzo ya moja kwa moja ili kujadilia hatma ya mateka wanaozuiliwa.
Kundi la Taleban linadai kuachiwa wapiganaji wao wanaozuiliwa katika jela nchini Afghanistan ndipo wawaachie mateka hao.Rais wa Afghanistan Hamid Karzai anakataa kutimiza dai hilo.Kundi hilo lilikuwa madarakani mwaka 96 hadi 2001 kabla ya kufurushwa na majeshi yanayoongozwa na Marekani ili kupambana na wapiganaji wa Al Qaeda wanaolaumiwa kutekeleza shambulio la mwaka huohuo nchini Marekani.