Kifo cha mhamiaji chazusha ghasia Australia
9 Novemba 2015Idara ya uhamiaji ya Australia imethibitisha kuwepo kile ilichokiita ''usumbufu mkubwa'' katika kituo hicho kilichoko kwenye kisiwa cha Christmas kinachomilikiwa na nchi hiyo. Waziri wa Uhamiaji wa Australia, Peter Dutton amesema ghasia hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali, ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Dutton amewaambia waandishi wa habari kwamba maafisa wanajadiliana na wahamiaji hao katika juhudi za kumaliza ghasia hizo na hivyo kurejesha hali ya utulivu. ''Kipaumbele chetu kwa sasa ni kuhakikisha tunarejesha utulivu ndani ya kituo na watu walioko kwenye eneo hilo wanaendelea na shughuli hizo,'' alisema Dutton.
Hata hivyo waziri huyo amekataa kufafanua zaidi kuhusu kile ambacho wahamiaji hao walikuwa wanakitaka. Amesema bado hafahamu ni wahamiaji wangapi wamehusika katika ghasia hizo.
Taarifa zinaeleza kuwa uzio wa kituo hicho umevunjwa na moto umewaka hali iliyosababisha wafanyakazi kukimbia. Hata hivyo, idara ya uhamiaji imethibitisha kutokea kwa ghasia kubwa, na kwamba wafanyakazi wake wameondolewa katika kituo hicho kwa sababu za kiusalama.
Ghasia zilizuka baada ya kifo cha mhamiaji mmoja
Mawakili wa wahamiaji hao wanaotafuta hifadhi Australia, wamesema ghasia zilizuka baada ya kuuawa kwa mhamiaji mmoja aliyejaribu kutoroka katika kituo hicho, siku ya Jumamosi. Kwa mujibu wa maafisa wa kituo hicho, kundi dogo la wahamiaji kutoka Iran lilianzisha maandamano ya amani kupinga kifo hicho.
Mbunge mmoja wa New Zealand, Kelvin Davis ambaye alikitembelea kituo hicho mwezi uliopita, amesema ghasia hizo zilizuka baada ya mmoja wa wahamiaji kuwauliza walinzi kuhusu kifo cha Fazel Chegeni, lakini alipigwa ngumi usoni.
Baadhi ya wahamiaji walianza kuharibu mali, ikiwemo kuanza kuchoma moto vitu kadhaa. Mwili wa mhamiaji huyo uliokotwa chini ya miamba katika ukingo wa bahari, na uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha kifo chake.
Katika miaka ya hivi karibuni Australia iliweka masharti magumu kwa wahamiaji wanaoomba hifadhi nchini humo, ambao wanaingia katika fukwe za nchi hiyo kinyume cha sheria. Kwa mujibu wa sera za nchi hiyo, watu wanaoomba hifadhi ambao wanawasili kwa kutumia boti, wanafanyiwa usaili katika kisiwa cha Christmas ambacho kimejitenga.
Waziri Mkuu wa New Zealand, John Key, amesema amearifiwa huenda kukawa na raia kadhaa wa nchi yake wanaohusika katika ghasia hizo, na kama ni kweli hawatofanya chochote kile katika kuwasaidia kuomba hifadhi kwa ajili yao nchini Australia.
Mmoja wa wahamiaji kutoka New Zealand, Lester Hohua, ameliambia shirika la utangazaji la Australia kwamba wahalifu waliohukumiwa ambao visa zao zilifutwa, walijiunga na wahamiaji wanaotafuta hifadhi kupinga namna wanavyotunzwa.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE
Mhariri: Yusuf Saumu