1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghasia zaongezeka siku moja kabla ya uchaguzi wa Afghanistan .

Halima Nyanza19 Agosti 2009

Wakati ikiwa imebaki siku moja kufanyika kwa uchaguzi wa Rais nchini Afghanistan kundi la wapiganaji la Taliban leo limeshambulia mji mkuu wa nchi hiyo Kabul ambao kwa sasa uko katika ulinzi mkali.

https://p.dw.com/p/JE4t
Rais anayetetea kiti chake nchini Afghanistan Hamid Karzai, anatarajiwa kushinda katika uchaguzi wa kesho kwa kiasi kikubwa.Picha: AP

Ulinzi wa Hali ya juu umeimarishwa katika juhudi za kuulinda mji mkuu wa Aghanistan Kabul, na mashambulio yanayofanywa na Taliban, baada ya mashambulio mawili ya kujitoa mhanaga na shambulio la roketi kukumba mji huo, siku moja kabla ya wananchi wa nchi hiyo kupiga kura kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo, siku ya kesho Alhamisi.

Jeshi la polisi nchini humo limewaua watu watatu waliokuwa na silaha, ambao wanadaiwa kuwa ni wapiganaji wa Taliban.

Kundi la Taliban nalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lililofanyika katika mji huo wa Kabul, ambalo wameliita kama sehemu ya mfululizo wa mashambulio yaliyopangwa kuhujumu hatua ya nchi za magharibi kuimarisha demokrasia, katika nchi hiyo ambayo ni moja wapo ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na utawala mdogo wa sheria duniani.

Mashambulio yalenga kuvuruga zoezi la Uchaguzi:

Aidha Mashambulio hayo yanaonekana kama yamelengwa kuchochea wasiwasi kwa Waafghanistan, kama itakuwa kuna usalama kwao kutoka nje na kwenda kupiga kura, licha ya kuhakikishiwa ulinzi mkali na serikali, ambapo ni jana tu, kumeripotiwa shambulio la kujitoa mhanga lililoua mwanajeshi mmoja wa NATO na Wa Afghanistan wengine wanane wakiwemo wafanyakazi wawili wa Umoja wa Mataifa.

Mwanajeshi huyo ambaye ni wa Marekani ni wanne kuuawa katika jeshi la NATO katika ghasia zilizotokea jana, ambapo pia wafanyakazi wawili wanaohusika na uchaguzi waliuawa pia kusini mwa nchi hiyo.

Serikali ya nchi hiyo imetaka kuzimwa kutangwazwa kwa baadhi ya habari kwa kuhofia kwamba, kuripotiwa kwa ghasia kunaweza kuathiri idadi ya watu watakaojitokeza kupiga kura, ambapo tayari watu milioni 17 wamejiandikisha kupiga kura.

Lakini hata hivyo, taarifa hiyo ya serikali imepingwa vikali.

Ban Ki Moon awaasa wapiga kura:

Ban Ki Moon im UN Hauptquartier berichtet über anstehende Myanmar Reise
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kwa wingi.Picha: AP

Wakati huohuo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametoa wito kwa watu wote wenye uwezo wa kupiga kura kufanya hivyo hapo kesho, kwa lengo la kusaidia ujenzi wa demokrasia nchini humo. na kuwataka wadau wote katika uchaguzi huo kuhakikisha kwamba zoezi hilo linakwenda kama lilivyopangwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani ambaye wanajeshi wake wapo wakiwajibika nchini humo, alikuwa na haya kuhusiana na uchaguzi huo wa kesho.

Katika uchaguzi huo Rais anayetetea kiti chake Hamid Karzai ambaye anaungwa mkono na nchi za magharibi anatazamiwa kushinda kwa kiasi kikubwa na kuepukana na hali ya kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman