Ghasia zaendelea nchini Tunisia kwa siku ya nne mfululizo
19 Januari 2021Zaidi ya watu 600 walikuwa wamekamatwa kufikia jana Jumatatu kuhusiana na vurugu hizo ambapo vijana wamerushia mawe polisi ambao walijibu kwa kuwafyatulia gesi za kutoa machozi.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa nchi hiyo Kais Saied, rais huyo alitembelea mtaa wa Errafeh katika eneo la M'nihla, mkoani Ariana ambapo alikutana na kundi la raia wa eneo hilo. Katika taarifa iliyotolewa na ujumbe huo mjini M'nihla, Saeid alithibitisha kuhusu haki za raia wa Tunisia za ajira, uhuru, na uadilifu wa kitaifa na kutoa wito wa kutohujumu watu na mali.
Rais Saied aliongeza kusema kupitia waandamanaji hao anataka kuzungumza na raia wote wa Tunisia. Amesema anafahamu ni nanai anayetumia umaskini wao na kwamba hawapaswi kumruhusu mtu yeyote kutumia masaibu yao. Aliwaomba wasishambulie mali ya kibinafsi na umma na kuwakumbusha kwamba wanaishi kutokana na maadili mema na sio kwasababu ya wizi ama uporaji.
Ghasia hizo za umma zinakuja wakati wa mzozo wa kiuchumi uliaothiri watu wengi na athari za janga la virusi vya corona katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika linalotegemea utalii ambako umaskini umekithiri na kusababisha mfumko wa bei za bidhaa na ukosefu wa ajira. Katika ghasia za alfajiri ya leo Jumanne, mamia ya vijana katika mji mkuu wa nchi hiyo Tunis, walikabiliana na polisi katika wilaya kadhaa ikiwa ni pamoja na mji wa Ettadhamen viungani mwa mji huo mkuu.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa katika mji wa pili mkubwa nchini humo Sfax, waandamanaji walifunga barabara kwa kuteketeza magurumu . Ghasia pia ziliripotiwa katika miji ya Gafsa, Le Kef, Bizerte, Kasserine , Sousse na Monastir. Maandamano na makabiliano na polisi yametokea katika kilele cha miaka 10 tangu kuzuka kwa mapinduzi ya kudai demokrasia ya mwaka 2011 ambayo raia wengine wa Tunisia wanadai hayajawanufaisha.