Ghasia zaendelea katika miji ya Uingereza
10 Agosti 2011Manchester, Liverpool na Birmingham ni miji iliyoshuhudia ghasia kubwa kabisa jana usiku. Katika mji wa Manchester ambao ni wa tatu kwa ukubwa nchini Uingereza, polisi walipambana na vijana waliokuwa wakivunja maduka na kupora mali huku wengine wakitia moto duka moja la nguo. Katika mji wa Salford, ulio karibu na Manchester, vijana waliwarushia polisi matofali na walichomo moto majengo. Picha katika televisheni zimeonyesha maduka na magari yakiwaka moto. Naibu mkuu wa polisi katika jiji la Machester, Gary Shewan amesema, polisi wamekumbana na machafuko yasio ya kawaida kutoka makundi ya wahalifu waliokuwa na lengo moja tu - kusababisha vurugu kubwa. Anasema hajawai kuona ghasia za kiwango kikubwa kama hicho.
Nako kaskazini-magharibi ya Uingereza, katika mji wa Liverpool, wafanya ghasia waliyachoma magari mawili ya wazima moto na gari la afisa wa wazima moto. Hapo awali, kiasi ya vijana 200 walivunja maduka na walipora mali. Watu 113 wamekamatwa Manchester na Salford na wengine 50, katika mji wa Liverpool.
Mjini Birmigham katikati ya Uingereza, watu 3 walifariki baada ya kugongwa na gari wakati wa ghasia. Rafiki mmoja wa marehemu hao, ameiambia BBC kuwa watu hao walikuwa sehemu ya kundi lililokuwa likilinda eneo lao ili kuzuia uporaji. Kwa mujibu wa polisi, mtu mmoja amekamatwa na uchunguzi unafanywa kuhusu tukio hilo.
Kwa upande mwingine, mji mkuu London, kwa sehemu fulani ulikuwa shwari, baada ya kiasi ya polisi 16,000 kusambazwa mitaani ambako vijana waliojificha nyuso, walipora maduka na walitia moto magari, wakati wa usiku kwa siku tatu mfululizo. Hiyo jana, wafanyakazi walirejea nyumbani mapema na maduka yalifungwa na madirisha yalipigiliwa mbao. Hata mchezo wa kirafiki uliopangwa kwa leo usiku kati ya timu za kandana za Uingereza na Uholanzi, umefutwa na michezo mingine mitatu ya klabu, imeahirishwa kwa sababu ya ghasia za London na hofu ya machafuko zaidi kutokea.
Viongozi katika jamii wamesema, mzizi wa ghasia za London, jiji lenye watu milioni 7.8 wa kabila mbali mbali, ni pengo linalozidi kuwa kubwa kati ya matajiri na tabaka la wafanyakazi. Lakini wengi wanasisitiza kuwa sababu kuu ni tamaa ya waporaji hao.
Machafuko ya kwanza yalitokea Jumamosi katika eneo la Tottenham mjini London, baada ya maandamano ya kulalamika kuhusu mauaji ya mwanamume aliepigwa risasi na polisi, kutumiwa vibaya na wafanya ghasia. Waziri Mkuu David Cameroon aliefupisha likizo yake na familia nchini Italia, ameahidi kuchukua kila hatua ili kurejesha utulivu. Leo anaongoza mkutano wa pili wa kamati maalum inayoshughulikia mizozo. Bunge pia limeitwa kutoka mapumzikoni kujadili ghasia hizo.
Mwandishi:Martin,Prema/rtre
Mhariri:Abdul-Rahman