Ghasia za mashabiki zachafua sura ya kandanda
12 Juni 2016Mamia kadhaa ya mashabiki wa England na Urusi walipambana mjini Marseille , wakirusha chupa za bia na viti na kusababisha mabomu ya kutoa machozi kufyatuliwa kutoka kwa polisi wa kuzuwia ghasia ili kudhibiti ghasia hizo katika mitaa miembamba ya mji huo wa zamani wa bandari.
Baadaye , katika matukio ambayo yanaweza kusababisha vikwazo kutoka kwa shirikisho la soka la Ulaya UEFA, mashabiki wa kandanda wa Urusi waliwashambulia wenzao wa England ndani ya uwanja mjini Marseille wa Stade Velodrome muda mfupi baada ya firimbi ya mwisho kulia katika mchezo wao ambao umemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mashabiki wa England walilazimika kuweka vizuwizi kujikinga na mashambulizi hayo, wakati picha ya kushitua ya baba mmoja akijaribu kumlinda mwanae mdogo wa kiume wakati mashabiki waliokuwa wamejifunika nyuso wakiwapiga mateke na ngumi mashabiki waliokuwa wakikimbia waliokuwa karibu nae , ilisambaa na kuwaacha mashabiki wakikasirishwa na kushindwa kwa maafisa kuingilia kati.
Ugonjwa mbaya wa ghasia michezoni
Mamia ya mashabiki wakipambana mitaani wakibeba viti tayari kuvirusha na watu waliokuwa wametapakaa damu wakiwa vifua wazi walipambana na polisi, ugonjwa wa ghasia umerejea kwa nguvu zote katika mashindano hayo yanayofanyika nchini Ufaransa.
Karibu watu 20 wamefikishwa hospitali wakiwa na majeraha.
Timu ya Urusi italazimika kukabiliana na hatua ya kusubiri baada ya ghasia hizo. Miaka minne iliyopita Urusi ilichukuliwa hatua na kupewa adhabu ya kupunguziwa pointi sita kufuatia ghasia za mashabiki wake nchini Poalnd katika michuano ya Euro 2012.
Wakati huo huo , katika pwani ya bahari ya Mediterania , mashabiki wa Ireland ya kaskazini walihusika katika mapambano na wenyeji katika mji wa Nice ambapo watu saba walijeruhiwa.
UEFA yashutumu
Shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA limeshutumu matukio ya siku hiyo. "Watu wanaojihusisha na vitendo vya ghasia hawana nafasi katika kandanda," imesema taarifa ya UEFA.
Huduma za dharura mjini Marseille zimesema watu 31 walijeruhiwa katika ghasia za Jumamosi, ikiwa ni pamoja na mtu mmoja ambaye alipigwa na kuzirai, na shabiki mmoja wa Uingereza ambaye alipata mshituko wa moyo.
Wingu la gesi ya kutoa machozi ilitoa picha ya machafuko kama , licha ya kwamba ni ya kiwango kidogo, ikilinganishwa na yaliyotokea katika mji huo miaka 18 iliyopita wakati ghasia zilipozuka kwa siku mbili na usiku katika mchezo kati ya England na Tunisia katika kombe la dunia.
Matukio hayo yamesababisha hasira nchini Uingereza , ambako ghasia za michezoni zinafikiriwa ni jambo la enzi za zamani.
"Wana matatizo gani watu hawa ? Ni fadhaa kwa nchi ," aliandika katika ukurasa wa Twitter mshambuliaji wa zamani wa England Gary Lineker.
"Unasewa zungumzia kuhusu ukorofi wa polis, ama mashabiki wengine wanaosababisha matatizo, lakini inaonekana kutokea kila mara wanapokuwapo mashabiki wa England," amesema Lineker.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Isaac Gamba