1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wazidi kuongezeka

Admin.WagnerD13 Oktoba 2015

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amekiri kwamba huenda Ujerumani ikashindwa kulifikia lengo la kuwa na bajeti iliyosawazika mwaka ujao ,kutokana na gharama za wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1GnRN
Wafuasi wa kundi la Pegida wanaowapinga wakimbizi nchini Ujerumani
Wafuasi wa kundi la Pegida wanaowapinga wakimbizi nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/L. Dubrule

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amekiri kwamba huenda Ujerumani ikashindwa kuwa na bajeti yenye urari mwaka ujao kutokana na gharama za kuwahudumia wakimbizi.

Waziri Schäuble amesema kwamba Ujerumani inataka kuwa na bajeti iliyosawazika bila ya kuchukua mkopo mpya, ikiwa itawezekana. Amesema watu wamemuuliza kwa nini anasema ,ikiwa itawezekena kuwa na bajeti linganifu bila ya kuchukua mkopo?. Waziri Schäuble aljibu kwa kusema kwamba kwamba hajui.

Kwa mara ya kwanza ,tangu mwaka 1969 Ujerumani, mwaka jana iliweza kuwa na bajeti iliyokuwa na uwiano kwa sababu serikali haikuchukua mkopo mpya.

Serikali ya Kansela Angela Merkel inatumai kwamba bajeti kama hizo zitakuwa jambo la kawaida. Lakini gharama zinazotokana na idadi kubwa ya wakimbizi ambazo hazikutarajiwa zitasababisha mzigo zaidi katika mfuko wa serikali.

Waziri Schäuble amesema Ujerumani haijawahi kukabiliwa na changamoto kubwa kama hiyo katika muda wa miaka 65 iliyopita ya historia yake.

Deutschland Pegida Kundgebung in Dresden
Picha: Reuters/H. Hanschke

Wanaopinga wakimbizi watanda mitaani

Idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia Ujerumani imesababisha ghadhabu miongoni mwa makundi ya watu wanaowapinga wakimbizi hao. Maalfu ya watu wa kundi linaloupinga Uislamu jana walifanya maandamano katika mji wa Dresden ulioko mashariki mwa Ujerumani.

Watu wa kundi hilo linaloitwa "Pegida" wanaopinga kusilimishwa kwa bara la Ulaya ,hawakubaliani na sera ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ya kuwapa wakimbizi hifadhi.

Mwanzilishi mwenza wa kundi hilo Lutz Bachmann amewalaumu viongozi wa Ujerumani juu ya suala la wakimbizi. Amesema wanaoiongoza serikali wanawapeleka watu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Ulaya. Amewata wafuasi wake waifanye hali isiwe ya kuvutia kuja Ujerumani ili wakimbizi wasiombe hifadhi kwa ajili ya kutafuta maisha bora.

Watu wapatao 9000 walishiriki katika maandamano ya mjini Dresden ya kuwapinga wakimbizi. Polisi imearifu kwamba maandamano mengine yalifanyika katika miji midogo ya karibu ya Chemnitz na Leipzig.

Watetezi wa wakimbizi wapambana na Pegida

Katika mji wa Dresden watu wapatao 250 pia walifanya maandamano ili kuwakabili wanaowapinga wakimbizi. Mfuasi mmoja wa kundi linalopinga Uislamu barani Ulaya Pegida, alikamatwa na polisi.

Na mfuasi mwengine anaweza kufunguliwa mashtaka kwa kitendo cha kuonyesha kitanzi cha kunyongea watu kilichokuwa na majina ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Makamu wake Sigmar Gabriel. Kansela Merkel anaunga mkono thabiti sera ya kulegeza masharti ya kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.

Idadi ya wakimbizi wanaokuja Ujerumani imekuwa inaongezeka ,na baadhi ya watu wanatabiri, huenda idadi hiyo ikafikia Milioni moja au hata zaidi,mnamo mwaka huu.

Mwandishi:Mtullya abdu./Dpae, afp.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman