1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan yafuta mipango ya uwanja wa Olimpiki

17 Julai 2015

Mipango ya uwanja wa michezo ya Olimpiki ya mwaka wa 2020 mjini Tokyo, Japan itafanywa upya kwa sababu ya gharama zinazoendelea kuwa kubwa. Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe

https://p.dw.com/p/1G0h7
Shinzo Abe Tokio Japan Wahl Olympia 2020
Picha: AFP/Getty Images

Abe ameongeza kuwa uwanja huo hautakuwa tayari katika wakati unaofaa kwa Kombe la Dunia la Mchezo wa Rugby mwaka wa 2019. Serikali ya Japan imekuwa chini ya shutuma kali wakati gharama za ujenzi wa Uwanja mpya wa Kitaifa zikipanda hadi yeni bilioni 252, ambazo ni kama dola bilioni 2 za Kimarekani, ikiwa ni karibu mara mbili zaidi ya makadirio ya mwanzo ya yeni bilioni 130 "Gharama ya ujenzi imepanda sana na kulikuwa na shutuma kutoka kwa umma, wakiwemo wanariadha, kuhusu muundo huo, hali iliyonifanya kuamini kuwa hatutaweza kuandaa mchezo ambao kila mmoja katika nchi hii atasherehekea".

IOC Treffen in Monaco 08.12.2014 Yoshiro Mori
Waziri mkuu wa Zamani wa Japan Yoshiro Mori, ambaye ni mweyekiti wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020Picha: Reuters/E. Gaillard

Uwanja huo, ulioundwa na mchora ramani Zaha Hadid mwenye makao yako Uingereza na kufafanishwa na kofia ya mwendesha baiskeli, umekosolewa kwa kuwa wa gharama kubwa na usiofaa katika eneo unaopaswa kujengwa mjini Tokyo.

Lakini mchora ramani Tadao Ando aliyeongoza kamati iliyouchagua muundo wa Hadid amesema ongezeko la gharama ya mipango ya ujenzi wa uwanja huo sio kosa lake. Ando amesema anataka muundo huo ubakie tu kama ulivyochorwa "Kama tu nyinyi nyote, nataka kuuliza, mbona inagharimu yeni bilioni 252? Kwani hakuna mbinu za kupunguza gharama hiyo? ni kazi ya sanaa ambayo kila mtu kote ulimwenguni ataiona, kazi ambayo pia inapaswa kutimiza mahitaji ya michezo. Ni kitu kigumu mno. Nilidhani JAPAN ingefanikiwa na hilo wakati nchi nyingine nyingi zilishindwa".

Katibu mkuu wa kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia la mchezo wa Rugby Akira Shimazu amesema wamekasirishwa na tangazo kuwa uwanja huo hautatumika kwa dimba hilo lakini waziri mkuu Abe ameahidi kuhakikisha kuwa tamasha hilo linandelea kama ilivyopangwa mwaka wa 2019.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman