1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ghani na hasimu wake Abdullah wakaribia kupatana

Josephat Charo
1 Mei 2020

Tume ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO inayoongozwa na Marekani nchini Afghanistan inabana taarifa muhimu kuhusu mashambulizi ya kundi la Taliban, shirika moja la serikali ya Marekani limesema Ijumaa (01.05.2020).

https://p.dw.com/p/3bfBc
Aschraf Ghani und Abdullah Abdullah
Picha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Awali tume hiyo ilikuwa ikifichua taarifa kuhusu mashambulizi yaliyofanywa na adui, mojawapo ya vipimo vya maoni ya umma vilivyobaki kuhusu mzozo huo na nguvu ya Taliban na makundi mengine ya uasi.

Katika ripoti yake inayotolewa kila baada ya miezi minne, afisi ya Inspekta Jenerali kwa ajili ya kuijenga upya Afghanistan ilisema tume hiyo sasa imeacha kutoa takwimu. Badala yake ilitoa taarifa fupi ikitambua Taliban imeongeza mashambulizi mwezi Machi, mara baaada ya kutiwa saini mkataba kati ya Marekani na Taliban ambao ulinuiwa kuyafungulia mlango mazungumzo ya amani.

Tume ya NATO imemwambia Inspekta Jenerali kwa ajili ya kuijenga upya Afghanistan SIGAR kwamba iliamua kubana taarifa kwa sababu mashambulizi ya adui ni suala nyeti katika mazungumzo kuhusu mashauriano ya kisiasa kati ya Marekani na Taliban. Inspekta Jeneral ametambua kwamba wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilisema huenda ikazitoa taarifa hizo katika siku za usoni.

Ripoti hii imetolewa huku uhasama mkali kati ya rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani, na hasimu wake, Abdullah Abdullah, ukionekana kukaribia kupataiwa ufumbuzi baada ya Abdallah kusema wamepiga hatua katika mazungumzo yao. "Tumepiga hatua katika mashauriano na tumeafikiana juu ya kanuni mbalimbali. Kazi ya kukamilisha taarifa za kina inaendelea kuyakamilisha makubaliano," Abdullah aliandika katika ukurasa wake wa twitter.

Ofisi ya Ghani haikutoa kauli mara moja kuhusu suala hilo.

Makamu wa pili wa rais wa Ghani, Sarwar Danish, amethibitisha kwamba Abdullah ataliongoza baraza la amani la kitaifa.

Taliban yaua maafisa 13 wa usalama

Wakati haya yakiarifiwa wanamgambo wa kundi la Taliban wamewaua maafisa 13 wa vikosi vya usalama vya Afghanistan katika mkoa wa kaskazini wa Balkh. Maafisa wengine 17 wamejeruhiwa katika hujuma hiyo wakati wapiganaji wa Taliban walipoishambulia wilaya ya Zareh mkoani humo usiku wa kuamia Ijumaa, madiwani wa mkoa Sakhi Lala na Mohammad Amin Dara-e Sufi wameliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa.

Afghanistan Kabul | Taliban werden aus dem Bagram Gefängnis entlassen
Wafungwa wa Taliban walioachiwa huru kutoka jela la BagramPicha: Reuters/National Security Council of Afg

Taliban wameongeza mashambulizi yao katika siku za hivi karibuni katika mikoa kadhaa ya kaskazini mwa Afghanistan, licha ya serikali na kundi hilo kuwaachia huru wafungwa kwa mujibu wa makubaliano na Marekani yaliyosainiwa mnamo mwezi Februari mjini Doha, Qatar.

Siku ya Jumatano Taliban waliwaua wapiganaji wapatao tisa wa vikosi vya uasi katika mkoa wa kaskazini wa Samangan, kwa mujibu wa maafisa.

Watoto zaidi ya milioni saba kukabiliwa na uhaba wa chakula

Kwingineko shirika linalotoa misaada kwa watoto Save the Children limesema watoto takriban milioni 7.3 wa Afghanistan huenda wakakabiliwa na uhaba wa chakula mwezi Mei kutokana na janga la virusi vya corona. Shirika hilo limesema kufungwa kwa shughuli nyingi katika miji mikubwa ya Afghanistan kumesababisha bei za ngano, mafuta na maharagwe kote nchini kupanda katika mwezi uliopita.

Mkuruenzi wa shirika la Save the Children nchini Afghanistan, Timothy Bishop, amesema, "Tunachohitaji ni jumuiya ya kimataifa kupeleka haraka mahitaji ya chakula nchini kwa ajili ya kusambazwa kwa jamii zinazokabiliwa na kitisho, wakiwemo watoto, akina mama wajawazito, wazee, watu wanaokabiliwa na utapiamlo na wagonjwa."

Serikali ya Afghanistan siku ya Alhamisi ilitangaza mpango wa majaribio wa usambazaji chakula katika mji mkuu, Kabul, unaojumuisha mikate ya bure kupitia maduka yanayooka na kuuza mikate.

(afp, dpa, ap)